Mafuriko Sudan yasababisha mfumuko wa bei ya bidhaa kwa asilimia 400:OCHA 

2 Oktoba 2020

Sudan inakabiliwa na zahma mbili kubwa ya mafuriko na mfumuko wa bei kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA. 

Katika taarifa yake iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi shirika hilo linasema zaidi ya watu 860,000 nyumba zao zimesambaratishwa au kuharibiwa na mafuriko, huku shule na vituo vya afya navyo vimeharibiwa kwa kiasi kikubwa hasa Kaskazini mwa Darfur, Khartoum, Darfur Magharibi na Sennar. 

Na kana kwamba mafuriko hayatoshi msemaji wa OCHA Jens Laerke amesema sasa changamoto nyingine kubwa imejitokeza ya mfumuko wa bei ambapo bei za bidhaa zinazozalishwa katika maeneo hayo imepanda kwa asilimia 300 hadi 400 na kuathiri vibaya mipango ya msaada kwa waathirika. 

Ameongeza kuwa mashirika yanayotoa msaada wa fedha taslimu kwa familia za waathirika sasa yanahitaji kubadilisha kiwango cha fedha wanazotoa kila wakati. 

Na bei ya wastani wa mlo wa  siku wa familia imeongeza kwa zaidi ya asilimia 200 hivyo kusababisha ugumu wa watu kumudu mahitaji ya msingi ya chakula. 

Hata hivyo OCHA inasema mashirika ya Umoja wa Mataifa na washirika wengine wa misaada ya kibinadamu wanaendelea kuwasaidia waathirika wa mafuriko na hadi sasa wameshawafikia watu 400,000 na misaada ya lazima lakini mfumuko wa bei na upungufu wa bidhaa za msingu vimekuwa vikwazo vikubwa kwa mikakati na msaada kwa waathirika. 

 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter