Awali lita 600 za maziwa ziliharibika, Benki ya Dunia imetuondolea adha hii: Mnufaika mradi wa PRAPS 

2 Oktoba 2020

Mafunzo, mtaji na vifaa kutoka Benki ya Dunia vimesaidia wafugaji kwenye taifa la Mali lililoko ukanda wa Sahel barani Afrika kuweza kuboresha miradi yao ya ufugaji kwa kuongeza thamani ya bidhaa na hivyo kuinua familia zao. 

Mradi huo wa Benki ya Dunia kwa wafugaji na wakulima Sahel, PRAPS umenufaisha wakazi 20,700 akiwemo Seydou Coulibaly ambaye ni mfugaji wa ng’ombe wa maziwa. 

Akiwa kwenye zizi lake lenye ng’ombe kadhaa wa maziwa, Seydou anasema kuwa awali hawakuwa na magudulia mahsusi ya kuhifadhi maziwa wanayokamua jioni kitu ambacho kilisababisha lita nyingi za maziwa kuharibika kila siku. 

“Kuna wakati tulipoteza lita 600 za maziwa. Lakini leo hii shukrani kwa mradi wa PRAPS tunaweza kuhifadhi maziwa kwa siku kadhaa bila hofu yoyote. Msaada huu umenipatia motisha sana katika kazi yangu. Kwa kutumia pikipiki  ya magurudumu matatu au guta, niliyopata kwenye mradi huu, sasa naweza kupeleka maziwa katika kituo cha kukusanya maziwa. Nilipatiwa pia vifaa vingine vya kuendeleza biashara yangu.” 

Maziwa wanapeleka kituo cha Koutiala ambako yanachakatwa katika bidhaa mbalimbali. 

Oumou Camara, naye mnufaika wa PRAPS, ni  mfanyakazi katika kituo hicho na anasema wanatumia maziwa kutegeneza jibini na maziwa mgando na kwamba, “siyo tu tunatumia kifaa kuua vimelea kwenye maziwa ili yakae muda mrefu, bali pia hatuna tena hofu ya kwamba maziwa yataharibika iwapo hatutauza bidhaa zetu ndani ya saa 24. Hata gharama za umeme zimepungua, kwa sababu sasa tuna umeme wa sola unaotumika kwenye kituo chote.” 

Oumou anasema kituo hiki cha kuuza maziwa kinamwezesha mno kiasi kwamba si mtegemezi tena wa fedha nyumbani na anagharamia mahitaji yote ili aweze kuhudumia vyema watoto wake. 

Asimilia 88 ya wanufaika 22,700 wa mradi huo wa PRAPS wa Benki ya Dunia ni wanawake. 

 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter