Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kushuhudia tabasamu baada ya majonzi ni kitu cha kipekee- Mshindi wa tuzo ya Nansen 2020 

Mayerlín Vergara Pérez, mshindi wa Tuzo ya Nansen mwaka 2020 inayotolewa na UNHCR, akimkumbatia msichana mdogo huko Riohacha, La Guajira, Colombia.
© UNHCR/Nicolo Filippo Rosso
Mayerlín Vergara Pérez, mshindi wa Tuzo ya Nansen mwaka 2020 inayotolewa na UNHCR, akimkumbatia msichana mdogo huko Riohacha, La Guajira, Colombia.

Kushuhudia tabasamu baada ya majonzi ni kitu cha kipekee- Mshindi wa tuzo ya Nansen 2020 

Msaada wa Kibinadamu

Mayerlín Vergara Pérez kutoka Colombia ndiye mshindi wa mwaka huu wa tuzo ya Nansen inayotambua watu waliojitolea kwa hali na mali kusaidia wakimbizi na watu wasio na utaifa. Mayerlin, yeye aliamua kuwa jukumu lake ni kusaidia watoto kuondokana na ukatili wa kingono.

Mayerlín Vergara Pérez, al maarufu, Maye,  mwenye umri wa miaka 45, amesaidia mamia ya watoto ya watoto kupitia shirika lisilo la kiserikali nchini Colombia Fundación Renacer. 

Watoto hao huwa wamenasuriwa kutoka mitaani, madanguroni au kwenye baa ambamo wanatumiishwa kingono, au hata wakati mwingine kusafirishwa kiharamu na wakati mwingine wanakuwa wamenusuriwa kutoka familia katili na hivyo mikononi mwa Maye ni kimbilio baada ya kupitia kiwewe. 

Ratiba ya kila siku inahusisha kukutana na mtu mmoja mmoja, makundi na pia kuwaelimisha. 

Akizungumzia kile anachokiona anapokutana nao, Maye anasema, “wako hatarini sana. Wanakuja kwetu wakiwa na machungu mengi, huzuni na hawana matumaini. Na nyumba yetu imekuwa nafasi, kimbilio ambamo wanakuwa huru na wanaweza kufanya lolote hata kukosea. Wanaweza kuanguka na kisha kusimama tena.” 

Katika shirika hili kuna wataalamu mbalimbali wakiwemo walimu, wanasaikolojia, wafanyakazi wa kijamii, wanasihi, wataalamu wa lishe na wanasheria, wote wakilenga kusaidia watoto kujenga upya maisha yao, kipindi ambacho huchukua takribani mwaka mmoja na nusu. 

Pindi baada ya kurejea katika hali ya kawaida watoto wanaanza tena masomo na katika kipindi chote cha miaka 32 cha shirika la Fundación Renacer, watoto wengi wamejikuta wakifanikiwa maishani. 

Kwa Maye hatua hii ni nzuri sana kwani anasema, “kuona huzuni yao inabadilika kuwa tabasamu, kuona hisia hasi zinageuka kuwa ndoto nzuri, kwangu mimi ni jambo la kipekee mno.” 

Kwa sasa watoto wapatao 40 wanaishi kwenye nyumba ya ghorofa mbili, ambapo asilimia 80 kati yao ni watoto wa kike wakiwa ni wa jamii za asili za Wayúu na Yukpa, zilizoko mpakani mwa Colombia na Venezuela. 

Sherehe za kumzawadia Maye tuzo yake zitafanyika kwa njia ya mtandao tarehe 4 mwezi huu wa Oktoba kwa lugha ya kispaniola na tarehe 5 Oktoba kwa lugha ya kiingereza na matangazo yatakuwa  kupitia mitandao yote ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR

Hivi karibuni Maye alijitolea kufungua kituo kipya cha makazi kwenye mji wa mpakani na Venezuela wa La Guajira kaskazini mashariki mwa Colombia ambako kumeshuhudiwa kiwango kikubwa cha utumikishwaji watoto kingono. 

Makazi ya Riohacha yanayoendeshwa na Fundación Renacer yalianzishwa mwaka 2018 baada ya kubaini watoto wengi kwenye mpaka wa Venezuela na Colombia ambao walikuwa wanatumikishwa kingono. 

Tuzo ya wakimbizi ya Nansen inatokana na Kamishna wa kwanza wa UNHCR ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel kutoka Norway, Fridtjof Nansen.