Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa atoa ripoti ya kazi ya shirika  2020

1 Oktoba 2020

Ripoti ya kila mwaka ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu kazi za shirika imechapishwa leo. 

Na ndani ya ripoti hiyo Antonio Guterres ameainisha matokeo ya shirika hilo linaloadhimisha miaka 75 mwaka huu akiweka wazi ukosefu wa mshikamano katika kutatua changamoto za sasa zinazoikabili dunia na kutoa mapendekezo ya mtazamo mpya wa utawala wa dunia. 

“Leo hii Umoja wa Mataifa unafanya kazi kila siku usiku na mchana kote duniani na unasaidia kuokoa maisha ya mamilioni ya watu kila siku” ameandika Katibu Mkuu katika ripoti hiyo. 

Ripoti pia inasema zaidi ya wafanyakazi 36,000 wa sekretariati ya umoja wa Mataifa na wafanyakazi wengine zaidi ya 95,000 ambao ni wa kiraia wanafanya kazi katika maeneo 8 ya muhimu ndani ya program zaidi ya 35 kwenye nchi zaidi ya 140 kote duniani. 

Na kazi yao imefanikishwa kwa mchango wa dola bilioni 14.2 zikijumuisha bajeti ya kawaida ya dola bilioni 3, mchango wa operesheni za ulinzi wa amani wa dola bilioni 7.2 na michango ya kujitolea ambayo ni jumla ya dola bilioni 4. 

Guterres katika ripoti hiyo amesema wanawake na wanaume wanaofanya kazi kwenye Umoja wa Mataifa wanawasaidia wakimbizi na watu waliotawanywa milioni 80 na kuhakikisha kwamba zaidi ya wanawake na wasichana milioni 2 wanajikwamua kutoka kwenye matatizo yanayohusiana na ujauzito na kujifungua. 

UN News
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres

 

Operesheni za amani ya UN 

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu zaidi ya operesheni 40 za kisiasa na za ulinzi wa amani zikihusisha wanajeshi, polisi na raia 95,000 wanafanya kila liwezekanalo kufikia na kudumisha amani na ulinzi kwa raia. 

“Msaada wa masuala ya uchaguzi ambao tunautoa sasa unafikia nchi 60 kila mwaka na msaada kwa waathirika wa utesaji unafikia watu 40,000. Takribani waangalizi 750,000 wanafanya tathimini kila mwaka ili kulinda haki za binadamu, kuarifu kuhusu ukiukwaji na kuwafikisha wahusika kwenye mkono wa sheria.” Amesema mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa. 

Wakati huohuo Katibu Mkuu anaamini kwamba juhudi zote hizi hazitoshi kudhibito wimbi la hofu, chuki, pengo la usawa, umasikini na kukosekana kwa haki. 

Zaidi ya hapo mwanzoni mwa 2020, dunia imetikiswa vibaya na janga la corona au COVID-19 ambalo limeleta athari kubwa kwa kila mtu. 

TANZBATT 7/Ibrahim Mayambua
Walinda amani wanawake kutoka Tanzania wakiwa na wanawake na watoto wakazi wa Beni, nchini DRC.

 

“Janga hilo limedhihirisha ni jinsi hali dunia isivyo imara. Limeanika matatizo ambayo yamekuwa yakipuuzwa kwa miongo sasa”. Amesema Katibu Mkuu katika ripoti hiyo huku akizizitiza kwamba hata wakati kabla ya kuzuka janga la COVID-19 ilikuwa bayana kwamba dunia haikuwa na muda wa kuweza kutimiza malengo ya maendeleo endelevu SDGs ifikapo mwaka 2030 ambao ndio ukomo wake. 

“Sasa hivi tuko katika hatihati ya kutumbukia kwenye mdororo mkubwa wa kimataifa tangu vita vya pili vya dunia na anguko kubwa la kipato tangu 1870” Amesema Guterres akikumbusha kwamba nchi zote zinakabiliwa na mustakabali wa Pamoja na kwa mantiki hiyo mshikamano wa kweli na umoja vitasaidia kufikia malengo ya pamoja. 

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameelezea kukosekana kwa mshikamano katika dunia ya sasa na kutoa wito wa kuchukua mtazamo mpya wa utawala wa kimataifa kusaka uwiano wa kifedha na mifumo ya biashara, kufufua ushirikiano wa kimataifa, kuwa na usawa kwenye utandawazi, kulinga haki na utu kwa kila mt una kulinda mazingira. 

Janga la COVID-19 ni zahma kwa binadamu wote, lakini wakati huohuo linatupa fursa adimu ya kufanya mabadiliko katika mwenendo wa kujikwamu na janga hili.” Amesema Bwana Guterres. 

 

 

  

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud