Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 25 baada ya Beijing, kuna mafanikio lakini kasi ni ndogo- Phumzile

Nana Konadu Agyeman Rawlings, Mke wa Rais wa Ghana, akijibu maswali ya wanahabari wakati wa mkutano wa kimataifa wa wanawake uliofanyika Beijing, China mwezi Septemba mwaka 1995.
UN /Chen Kai Xing
Nana Konadu Agyeman Rawlings, Mke wa Rais wa Ghana, akijibu maswali ya wanahabari wakati wa mkutano wa kimataifa wa wanawake uliofanyika Beijing, China mwezi Septemba mwaka 1995.

Miaka 25 baada ya Beijing, kuna mafanikio lakini kasi ni ndogo- Phumzile

Wanawake

Azimio la Beijing na Jukwaa la kuchukua hatua vimefungua zama mpya ya kusaka usawa wa kijinsia, amesema Phumzile Mlambo-Ngcuka katika hotuba yake aliyotoa leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani wakati wa miaka 25 ya maadhimisho ya mkutano wa kimataifa wa wanawake, FWCW uliofanyika Beijing, China.
 

Bi. Ngcuka ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN-Women amesema, azimio hilo, “limeleta mabadiliko chanya makubwa ikiwemo marekebisho ya kisheria 274 katika mataifa 131. Wanawake zaidi hivi sasa wanashiriki kwenye michakato ya amani. Uhalifu wa kijinsia kwenye mizozo sasa unatambuliwa chini ya sheria za kimataifa na wahusika wanafunguliwa mashtaka. Maisha ya watoto wa kike na wanawake yamenufaika na ongezeko la kuandikishwa shuleni sambamba na huduma za uzazi.”

Akamulika pia wanawake kwenye uongozi wa juu akisema, “mwaka 1995, mjini Beijing walikuwepo wanawake 12 wakuu wa nchi na serikali na leo hii tuna wanawake 22 wakuu wa nchi na serikali katika mataifa 193.”

Hata hivyo amesema licha ya mafanikio hayo bado kuna changamoto ikiwemo kuwa mafanikio hayatoshelezi na pia kasi ni ndogo sana.

Amesema mathalani uongozi wa wanawake, ikiwemo wasichana ni muhimu sana wakati huu wa dharura ya kujenga upya jamii baada ya janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19, “wanawake na wakazi wa dunia wanataka mabadiliko haya.”

Mlinda amani kutoka Ethiopia aliyeko ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, akisindika kundi la wanawake kwenye kuchanja kuni nje ya kituo cha ulinzi wa raia, POC.
UNMISS\Nektarios Markogiannis
Mlinda amani kutoka Ethiopia aliyeko ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, akisindika kundi la wanawake kwenye kuchanja kuni nje ya kituo cha ulinzi wa raia, POC.

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UN-Women amesema katika muongo wa hatua uliobakia kuelekea ukomo wa 2030, hakuna tena kisingizio chochote katika ukosefu huo wa mizania kwenye uongozi.

Amesema ushirikiano wa kimataifa na Umoja wa Mataifa ni vitu muhimu, wanawake wanaamini kwenye hilo na hivyo ni lazima iwe jumuishi, “Wanawake hivi sasa wanataka kasi ya haraka zaidi kuelekea uwakilishi wa asilimia 50 kwa 50 katika nyanja zote kuanzia mabaraza ya mawaziri, bodi za mashirika kwenye uchumi ambako pia wanawake wajumuishwe kama wanufaika wa mipango ya kuchechemua uchumi baada ya COVID-19.”

Bi. Ngcuka amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameonesha utashi wa kisiasa na uamuzi thabiti kuanzia ngazi za juu za uongozi kwenye chombo hicho.

Hivyo amesema, tuko "katika njiapanda. Mustakabali unategemea ushiriki wa vizazi vyote, watu wa rangi zote na watu wenye uwezo mbalimbali ili kila pahali duniani, mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 10 mwaka 2020 aweze kuwa na ustawi bora kama msichana ifikapo mwaka 2030.”

Ameshukuru wale wote walioungana katika jukwaa la wadau mbalimbali la Kizazi cha Usawa, zikiwemo serikali, mashirika ya kiraia, sekta binafsi na wanaume na wavulana, viongozi na wenyeviti wenza wa jukwaa hilo ambao ni Ufaransa na Mexico.

Amekumbusha kuwa wanawake duniani wanaamini kwenye Umoja wa Mataifa na mashikamano na mataifa wanachama akisema wanaamini sote kwa pamoja “tunaweza kubadili mustakabali wetu ambao uko mikononi mwetu.”