Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Changamoto kwangu ni fursa ya kujifunza:Fiona Beine,UNAMI

Baghdad, Mji mkuu wa Iraq
UNAMI
Baghdad, Mji mkuu wa Iraq

Changamoto kwangu ni fursa ya kujifunza:Fiona Beine,UNAMI

Wanawake

Kutana na Fiona Beine mmoja wa wanawake wanaotoa mchango mkubwa katika operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa. Hivi sasa yeye ni naibu mshauri wa masuala ya usalama kwenye kwenye idara ya usalama ya mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq UNAMI. 

Fiona Bine ni raia wa Uganda akiwa katika eneo lake la kazi mjini Baghdad nchini Iraq anasema yeye ni mtu anayependa kukabili changamoto kwa sababu zinampa mafunzo katika maisha yake. 

Fiona ni miongoni mwa mamia ya wanawake kutoka nchi mbalimbali wanaohudumu katika nyadhifa za juu kwenye operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa. 

Na Umoja wa Mataifa umewapa nafasi wanawake kama yeye kwa sababu unaamini kwamba mchango wao katika kusaka amani ni mkubwa, kwasababu unafanya mikataba ya amani kuwa imara, jamii kuwa na mnepo na uchumi kunawiri. 

Fiona anasema safari yake ilianzia nyumbani Uganda mara tu alipohitimu masomo ya Chuo kikuu, “nilienda moja kwa moja kufundisha na shule niliyofundisha ilikuwa inaendeshwa na jeshi, hivyo hapo nilipata mwanga wa jinsi majeshi yanavyofanya kazi na nikaona kwamba hiyo ni fursa nzuri kwangu kikazi kujaribu tasnia mpya.” 

Mshauri huyo wa usalama ambaye anasimamia masuala ya utawala na msaada anasema ingawa kwenda Iraq kama ilivyo sehemu nyingine yoyote yenye migogoro ni mtihani mkubwa aliona pia kwake ni fursa ya kipekee. 

“Kila mtu anajua kwamba haya ni mazingira ya kazi yenye changamoto lakini nadhani shirika limeyafanya mazingira ya kazi kuwa bora. Kwa mfano malazi na ustawi wa wafanyakazi na viongozi wetu wamekuwa wakitusaidia kwa mfano kunipa likizo hata wakati ambao haikupangwa. Ni uzoefu mzuri na wenye changamoto ambao pia unatoa fursa nzuri za kazi.” 

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa wanawake kama Fiona huwa ni mfano wa kuigwa mashinani na wanaweza kuwachagiza wanawake na wasichana katika jamii zenye mfumo dume kupigania haki zao ndio maana unafanya juu chini kuhakikisha idadi ya wanawake kwenye operesheni za amani inaongezeka.