Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tumeona mafanikio miaka 25 baada ya Beijing, licha ya changamoto- Mongela

Getrude Mongela, Katibu Mkuu wa mkutano wa 4 wa kimataifa wa wawanake uliofanyika Beijing, China mwaka 1995.Hapa alikuwa anahojiwa na Stella Vuzo wa UNIC Dar es salaam.
UN Tanzania/Ahimidiwe Olotu
Getrude Mongela, Katibu Mkuu wa mkutano wa 4 wa kimataifa wa wawanake uliofanyika Beijing, China mwaka 1995.Hapa alikuwa anahojiwa na Stella Vuzo wa UNIC Dar es salaam.

Tumeona mafanikio miaka 25 baada ya Beijing, licha ya changamoto- Mongela

Wanawake

Hii leo mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA75 unakuwa na kikao cha ngazi ya juu kuhusu kuchagiza utekelezaji wa usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake na mtoto wa kike, sambamba na maadhimisho ya miaka 25 tangu mkutano wa 4 wa kimataifa kuhusu wanawake uliofanyika Beijing nchini China mwaka 1995. 

Katika mkutano huo wa Beijing, washiriki kutoka nchi maskini na tajiri walipitisha mwongozo wa utekelezaji wa Beijing wenye kurasa 129 na vipengele 12 vya kuzingatia. 

Mambo hayo ni umaskini, elimu na mafunzo, afya, ghasia, mizozo ya kivita, uchumi, madaraka na upitishaji maamuzi, mifumo ya kitaasisi, haki za binadamu, vyombo vya habari, mazingira na mtoto wa kike. 

Wanafunzi wa wakiwa darasani katika shule ya msingi ya Zanaki jijini Dar es Salaam tanzania
World Bank / Sarah Farhat
Wanafunzi wa wakiwa darasani katika shule ya msingi ya Zanaki jijini Dar es Salaam tanzania

Katibu Mkuu wa mkutano huo wa Beijing alikuwa Getrude Mongela ambaye Stella Vuzo wa kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa, UNIC nchini Tanzania amemuuliza, miaka 25 baada ya mkutano hali iko vipi? Bi Mongela anasema, “miaka 25 sasa imepita tumeangalia yote tuliyokubaliana Beijing, tumeona tumepiga hatua kiasi gani. Inapokuja kwenye suala kama elimu, mataifa mengi yamekubaliana kutekeleza usawa kati ya mtoto wa kike na wa kiume. Na Tanzania nadhani tumefanya kazi nzuri zaidi, na jambo ambalo limenifurahisha zaidi rais wetu na serikali yake ya awamu ya 5, wamechukua uamuzi wa kuhakikisha watoto wote wa shule hawalipi karo tangu wanapoanza shule hadi anapomaliza kidato cha 4. Watu wengi labda hawajui, hayo ni mapinduzi makubwa. Tuliposoma sisi, tatizo lilikuwa moja asomeshwe mtoto wa kike au wa kiume.” 

Wakati wanawake wametoka mbali tangu kupitishwa kwa Jukwaa la Hatua la Beijing karibu miaka 25 iliyopita, bado wako nyuma kwa karibu kila lengo la Maendeleo Endelevu (SDG).
UN Women India
Wakati wanawake wametoka mbali tangu kupitishwa kwa Jukwaa la Hatua la Beijing karibu miaka 25 iliyopita, bado wako nyuma kwa karibu kila lengo la Maendeleo Endelevu (SDG).

Je kwa upande wa nchi nyingine za Afrika ?, “wenzetu wa nchi za Afrika magharibi wengi wamejiimarisha katika uchumi. Mwanamke ana uchumi na ana uwezo .Wenzetu huko Nigeria unakuta mwanaume ameoa wanawake wanne, na si kwamba awatunze, wamtunze yeye. Kwa hiyo kuna mabadiliko mengine si mazuri sana lakini inaonesha uwezo wa mwanamke kiuchumi na haya yamefanyika kwenye maeneo mengi.” 

Soundcloud

 

Bi. Mongela akazungumzia pia nchi za magharibi, "pia walikuwa na matatizo, tulipoenda Beijing, ilikuwa malipo ya mwanamke wanafanya kazi ile ile, ni mwalimu kama mwalimu wa kiume lakini mwalimu wa kiume atalipwa zaidi kuliko mwalimu wa kike, au daktari wa kiume atalipwa zaidi kuliko daktari wa kike. Hayo nayo yamesawazishwa. Tumekuwa na hatua mbalimbali kila sehemu lakini bado tuna changamoto. » 

Mkutano wa kwanza wa kimataifa wa wanawake ulifanyika Mexico City nchini Mexico mwaka 1975, wa pili ulifanyika Copenhagen, Denmark mwaka 1980 na kisha Nairobi Kenya mwaka 1985 na miaka 20 baadaye Beijing China mwaka 1985.