Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wazee lazima wawe kipaumbele katika juhudi zetu za kuishinda COVID-19-Guterres  

Wanawake wazee katika moja ya kambi ya wazee inayohudumiwa na serikali nchini Msumbiji.
World Bank/ Eric Miller
Wanawake wazee katika moja ya kambi ya wazee inayohudumiwa na serikali nchini Msumbiji.

Wazee lazima wawe kipaumbele katika juhudi zetu za kuishinda COVID-19-Guterres  

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ulimwengu unaadhimisha miaka 30 ya Siku ya Wazee duniani tunapotathimi athari mbaya na kali ambazo janga la COVID-19 limesababisha kwa wazee ulimwenguni kote, sio tu kwa afya zao, bali pia juu ya haki zao na ustawi wao, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ujumbe wake alioutoa hii leo kuhusu Siku ya leo ya Kimataifa ya wazee duniani na kisha akashauri.  

“Wazee lazima wawe kipaumbele katika juhudi zetu za kuishinda COVID-19. Kulingana na mada ya maadhimisho ya mwaka huu, lazima pia tuchunguze jinsi janga hilo linavyoweza kubadilisha jinsi tunavyoshughulikia umri na uzee katika jamii zetu. Kupanua fursa kwa wazee na kuongeza ufikiaji wao wa afya, malipo ya uzeeni na ulinzi wa jamii vitakuwa muhimu.”   

Aidha Bwana Guterres amesema wakati ulimwengu unapotafuta kupona vizuri kwa pamoja, lazima wanadamu wafanye juhudi za pamoja katika kipindi cha miaka kumi kilichopewa jina muongo mmoja wa kuzeeka kwa afya yaani mwaka 2020 hadi 2030 kuboresha Maisha ya wazee, familia zao na jamii, “uwezo wa wazee ni msingi mzuri wa maendeleo endelevu. Zaidi ya hapo awali, lazima tusikilize sauti zao, mapendekezo na mawazo ili kujenga jamii jumushi na rafiki.” 

Naye Claudia Mahler ambaye ni Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu wazee kufurahia haki zote za binadamu, ametoa wito kuwapa kipaumbele wazee katika kipindi hiki cha dunia kurejea katika hali yake baada ya COVID-19 na hata baada ya hapo. 

Kupitia ujumbe wake alioutoa hii leo kuhusu siku hii ya kimataifa ya wazee Bi Mahler amesema wazee wana majukumu kadhaa muhimu katika jamii ikiwemo kulea, kujitolea na viongozi wa jamii. Mchango muhimu wa wazee katika kushughulikia janga ikiwemo kama wahudumu wa afya na walezi, mara nyingi hupuuzwa na kunatakiwa kutambuliwa.