Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kulinda bayonuai ni jukumu la kila mtu kwa ajili ya kizazi hiki na vijavyo: Mrema

Elizabeth Maruma Mrema, Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Mkataba wa Kimatafa wa Bayonuai ya kibaiolojia, CBD.
© FAO/Pier Paolo Cito
Elizabeth Maruma Mrema, Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Mkataba wa Kimatafa wa Bayonuai ya kibaiolojia, CBD.

Kulinda bayonuai ni jukumu la kila mtu kwa ajili ya kizazi hiki na vijavyo: Mrema

Tabianchi na mazingira

Mkutano wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaendelea mjini New York Marekani na leo unajikita na suala la bayonuai ambayo kwa muda sasa imekuwa ikiendelea kupotea na kuzusha hofu ya mustakbali wa viumbe vya dunia wakiwemo binadamu, mazingira na sayari yenyewe kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo.  

Mada kuu inayojadiliwa katika mkutano wa leo uliowaleta pamoja nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ni, “hatua za haraka kuhusu bayoanuai kwa ajili ya maendeleo endelevu”.  

Miongoni mwa wazungumzaji wakuu wa mjadala wa leo ni Bi. Elizabeth Mrema katibu mtendaji wa mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya bayonuai. Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa ameanza kwa kueleza ni kwa nini suala hilo linapaswa kupewa uzito wa hali ya juu na hasa sasa kuliko wakati mwingine wowote.  

"Ni kweli kabisa kwamba binadamu wakati huu tumesimama njiapanda kuhusu urithi tunaowaachia vizazi vijavyo. Ushahidi wote wa kisayansi umeonyesha ukweli kwamba bayonuai inapungua kwa kiasi ambacho hakijapata kutokea na shinikizo zinazosababisha kupungua huku bado zinaendelea kuongezeka kwa mfano janga tulilonalo la COVID-19 limeangazia zaidi mahusiano kati yetu na maumbile au bayonuai.” 

Zipi zingine zinaweza kuwa athari kubwa kama hatua hazitochukuliwa wakati huu? 

“Itapunguza uwezo wa bayonuai na mifumo ya ikolojia kutoa huduma muhimu za kuendeleza maisha, kuanzia usalama wa chakula, lishe kwa binadamu, ubora wa maji safi tunayopata kutoka kwa bayoanuai au hata magonjwa. Tumeingilia mapori nah ii imesababisha magonjwa kutoka kwa Wanyama kuja kwa binadamu, kutoka binadamu na kusambaa na kujikuta wote tumefungiwa kama ilivyo sasa hivi. Virusi , vijidudu kama vya corona vimeibuka kutokana na Wanyama wa porini” 

Huko Belarus wanatumia mabwawa kama haya na kuyabadilisha yaweze kuinasa hewa chafuzi kutoka katika anga ili kuipunguza katika hewa
UNDP Belarus
Huko Belarus wanatumia mabwawa kama haya na kuyabadilisha yaweze kuinasa hewa chafuzi kutoka katika anga ili kuipunguza katika hewa

 

Kwa nini inakuwa ni vigumu kwa nchi kulizingatia hili na kulinda bayonuai? 

“Kwa kweli nchi nyingi na zote zinajitahidi sana , nafikiri kinachokosekana tunahitaji kupata kabisa utashi ule wa kisiasa toka kwa viongozi wetu wa juu kusaidia sekta zote zinazohusika moja, mbili bado nchi nyingi zinatoa ruzuku kubwa katika maeneo mengi ambayo hayasaidii bayoanuai zaidi yanaharibu bayonuai.” 

Unafikiri kuna uhusiano gani hasa uliopo baina ya maisha yetu ya kila siku na suala hili la bayonuai na maendeleo lakini pia katika kuhakikisha kwamba vizazi vijavyo havipotezi kila kitu 

Tutalaumiwa sana na vizazi vijavyo tusipoangalia, kulinda mazingira na kukomesha upotezaji wa bayonuai ni njia ya kufikia maendeleo endelevu. Kwa kulinda bayonuai tutachangia kufikia angalau malengo 11 kati ya 17 ya maendeleo endelevu” 

 Wadau hawa wakubwa tuseme serikali , makampuni, sekta binafsi na watu binafsi wafanye nini ili kuhakikisha wanasaidia katika kuokoa bayoanauai? 

“Bayonuai sio sekta ya idara ya mazingira peke yake ni sekta zote katika serikali na watu wote mimi na wewe hata huko majumbani kila mtu anatakiwa kuzingatia na pia kuweza kuchangia katika kulinda bayoanuai. 

Mkutano wa leo unatarajiwa kutoka na azimio ambalo litakuwa muongozo wa nchi zote wanachama kuendeleza ahadi zao na kuchukua hatua kwa ajili ya sasa na kwa baadaye.