Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNGA75 yafunga pazia, viongozi waahidi kudumisha ushirikiano wa kimataifa:PGA 

Volkan Bozkir, Rais wa mkutano wa 75 wa Baraza Kuu akitoa hotuba ya kufunga mjadala wa wazi wa Baraza Kuu, UNGA75.
UN Photo/Loey Felipe
Volkan Bozkir, Rais wa mkutano wa 75 wa Baraza Kuu akitoa hotuba ya kufunga mjadala wa wazi wa Baraza Kuu, UNGA75.

UNGA75 yafunga pazia, viongozi waahidi kudumisha ushirikiano wa kimataifa:PGA 

Masuala ya UM

Wakati mjadala wa kihitoria wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitia mtandaoni UNGA75 umefunga pazia leo, Rais wa Baraza Kuu la Umoja huo amesema viongozi wa kisiasa wameahidi kuonesha mshikamano wa kimataifa.

Kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya Umoja wa Mataifa viongozi wa dunia hawakuweza kukutana ana kwa ana kwa ajili ya mjadala wa Baraza Kuu unaofanyika kila mwaka , lakini Rais wa chombo hicho chenye wajumbe 1993 amesema tahadhari iliyolazimishwa na janga la corona au coronavirus">COVID-19, “haikuzuia ushirikiano wa kimataifa kufanya kazi yake kwa kiwango cha juu kabisa.” 

Rais huyo wa Baraza Kuu Volkan Bozkir akifunga mjadala huo wa ngazi ya juu wa 75 wa Baraza Kuu amesema, “Mkutano huu umekuwa wa muhimu na wa kipekee”. 

Uamuzi wa kihistoria wa Baraza Kuu uliofanyika mwezi Julai wa kuruhusu viongozi wa dunia kutuma ujumbe wao uliorekodiwa kwa njia ya video na kuhakikisha masharti ya kujitenga yanazingatiwa kwa watakaokutana ana kwa ana, ulimaanisha wajumbe wachache kwenye ukumbi wa Baraza Kuu mjini New York na kutokuwepo msongamano wa magari ambao kama ada hufurika kwenye eneo hilo la mashariki mwa Manhattan. 

Bozkir amesema na kwa kuruhusu kurekodi ujumbe kumesaidia wajumbe wengi zaidi kushiriki mjadala wa mwaka huu ambao ulijikita na mada mbalimbali kuanzia mshikamano unaotarajiwa sana kwa ajili ya chanjo ya COVID-19 na kufufua ushirikiano wa kimataifa hadi kuchagiza masuala ya usawa wa kijinsia, malengo ya maendeleo endelevu SDGs na hatua za mabadiliko ya tabianchi. 

Ameongeza kuwa wakuu wa nchi na serikali, pamoja na mawaziri kwa siku sita zilizopita wameainisha ajenda, “ambazo sio tu zinaunga mkono vipaumbele nilivyoviorodhesha lakini pia wametoa muongozo kuhusu hatua zinazohitajika kupambana na changamoto zinazotukabili.” 

Uwezo na umuhimu wa UN 

Rais Bozkir amesema “Ukweli kwamba viongozi wengi wa dunia walichagua kuhutubia Baraza hili ni Ushahidi wa uwezo na umuhimu wa Umoja wa Mataifa. Hakuna jukwaa linguine lolote kwenye kalenda ya kimataifa lenye uwezo wa kukusanya watu wote haw ana hakuna chombo kingine chohote chenye uwezekano wa kushughulikia changamoto za kimataifa kama Umoja wa Mataifa. Ingawa uwepo wao ulikuwa kupitia mtandao lakini viongozi wetu wa kisiasa wameonyesha dhamira yao katika ushirikiano wa kimataifa na Umoja wa Mataifa.” 

Kikao kingine cha mjadala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa iwe ni kwa njia ya mtandao au kukutana ana kwa ana kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa itakuwa hapo mwakani mwezi Septemba katika UNGA76.