Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 imetupa mafunzo-Uganda 

Balozi Philip Ochen Odida, Naibu Mwakilishi wa kudumu wa Uganda katika Umoja wa Mataifa akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA75
UN Photo/Loey Felipe
Balozi Philip Ochen Odida, Naibu Mwakilishi wa kudumu wa Uganda katika Umoja wa Mataifa akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA75

COVID-19 imetupa mafunzo-Uganda 

Afya

Tunauona ushirikiano wa kimataifa kama njia ya kushughulikia matishio magumu na mapya kama vile janga la COVID-19 ambalo limeathiri kila mwanachama wa jumuiya ya kimataifa, imeeleza sehemu ya kwanza ya hotuba ya Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda katika mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambayo imesomwa kwa niaba yake na Naibu Mwakilishi wa kudumu wa Uganda katika Umoja wa Mataifa, Balozi Philip Ochen Odida ikieleza pamoja na mengine, kile ambacho wamejifunza kutokana na ugonjwa huo. 

Akiendelea kueleza kuhusu janga la ugonjwa wa coronavirus">COVID-19, Rais Museveni ameeleza hatua ilizozichukua Uganda ili kupambana na ugonjwa huo unaosababishwa na virusi vya corona akieleza kuwa walianza kwa kutengeneza miongozo, upimaji, ufuatiliaji, karantini na tiba na pia kuzuia kukutana ili kudhibiti usambaaji.  

“Serikali pia imeendelea kuimarisha mfumo wake wa afya kama sehemu yake ya ahadi ya afya kwa wote katika kuhakikisha kuwa vituo vya afya ambavyo vinatoa huduma kwa wagonjwa wa COVID-19 vinakuwa na vifaa vyote muhimu ili kusaidia udhibiti wa ugonjwa kwa usahihi.”  Amesema.  

Aidha hotuba ya Museveni imeipongeza jumuiya ya kimataifa akiutaja Umoja wa Mataifa, Muungano wa Afrika, AU, Jumuiya ya Madola, Jumuiya ya Afrika Mashariki  na mengine, kwa namna walivyolishughulikia janga. Katika kipengele hicho ha shukrani, Uganda pia imetambua mchango wa shirika la fedha duniani, IMF, Benki ya dunia na mataifa mengine yaliyoendelea kwa kusitisha kwa muda ulipaji wa madeni kwa nchi 76 kwa kipindi cha mwaka mmoja.  

COVID-19 imetupa mafunzo kadhaa  

Hotuba ya Rais Museveni imeeleza kuwa, “kwanza imeonesha namna dunia yetu ambavyo imeunganishwa na kutegemeana. Pili lazima tuukumbatie wakati wa dijitali na teknolojia zaidi kwa uzalishaji na huduma kama vile benki, kuuza tena, na ujifunzaji, na pia huduma za umma. Tatu, taasisi nyingi zina uwezo wa kujibadilisha na kufanya mambo mengine. Nchini Uganda, viwanda vya nguo vimeanza kutengeneza barakoa, Vyuo vikuu vimeanza kutengeneza mashine za kusaidia kupumua, viwanda vya sukari vinatengeneza vitakasa mikono.” 

Ugaidi bado ni tishio 

Vile vile hotuba ya Rais wa Uganda imezungumzia tishio la ugaidi duniani kuwa bado linasalia kuwa changamoto ya usalama na kwamba madhara ya COVID-19 yanaweza kusaidia vitendo vya ugaidi kushamiri.  

“Uganda inasalia kuunga mkono juhudi za ulimwengu n aza kikanda katika kudhibiti ugaidi. Katika ukanda wetu wenyewe, makundi ya kigaidi kama vile Al-Shabaab, Boko Haram, ISIS, Al Qida na ADF yanaendelea kuwa tishio kwa usalama wetu wa pamoja na maendeleo. Kuyadhibiti maundi haya kunahitaji ushirikiano na hatua thabiti.” Amesisitiza Rais Museveni.  

Katika kuhitimisha, hotuba ya Museveni imerejelea wito wa kuboresha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kuwa na uwakilishi linganifu hususani kwa kulipa nafasi bara la Afrika ambalo masuala yake mengi ndiyo yanakuwa katika ajenda za Baraza hilo wakati bara lenyewe likikosa kuwa na uwakilishi.