Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yachunguza madai ya ukatili wa kingono kwenye operesheni dhidi ya Ebola

Mhudumu wa afya akimchunguza mtoto aliyebebwa na mlezi iwapo ana Ebola au la kwenye kituo cha kutibu Ebola huko Beni, jimboni Kivu Kaskazini nchini DR Congo. (24 Machi 2019)
© UNICEF/Vincent Tremeau
Mhudumu wa afya akimchunguza mtoto aliyebebwa na mlezi iwapo ana Ebola au la kwenye kituo cha kutibu Ebola huko Beni, jimboni Kivu Kaskazini nchini DR Congo. (24 Machi 2019)

WHO yachunguza madai ya ukatili wa kingono kwenye operesheni dhidi ya Ebola

Haki za binadamu

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO limesema linachunguza madai ya kuwepo kwa utumikishaji wa kingono wanawake na wasichana wakati wa operesheni za kukabiliana na mlipuko wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
 

Taarifa ya WHO iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi inasema, “WHO, uongozi wake na wafanyakazi wameshtushwa na ripoti hizo za karibuni zikidai kuwepo utumikishaji na unyanyasaji wa kingono. Vitendo hivyo vimefanywa na watu wanaodai kujitambulisha kuwa wafanyakazi wa WHO na havikubaliki na vitachunguzwa kwa kina.”

WHO imesema “usaliti wa watu kwenye jamii ambazo tunahudumia ni kosa kubwa. Hatutaki kuvumilia tabia hiyo miongoni mwa wafanyakaiz wetu, makandarasi au wadau wetu.”

Shirika hilo limesema kuwa yeyote atakayebainika kuhusika na vitendo hivyo atawajibishwa na kukabiliwa na hatua kali ikiwemo kufukuzwa kazi mara moja.

Tayari Mkurugenzi Mkuu wa WHO ameanzisha tathmini ya kina dhidi ya madai hayo.

Shirika hilo limesisitiza kuwa lina sera ya kutovumilia kabisa ukatili na unyanyasaji wa kingono.

Taarifa za madai hayo ya ukatili wa kingono zimechapishwa na shirika moja la habari zikifuatia uchunguzi wa takribani mwaka mmoja ambamo wanawake 51 wamedai kunyanyaswa au kukumbwa na ukatili wa kingono na watu waliojidai kuwa wahudumu wa kibinadamu huko Beni, jimboni Kivu Kaskazini.