Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Si haki kwa watu milioni 690 kulala njaa wakati chakula kinatupwa kila uchao:UN

Mradi wa FAO wa uhakika wa chakula (PESA) katika sekta ya kilimo, mifugo, maendeleo vijijini, uvuvi na kilimo
© FAO-Magnum Photos/Alex Webb
Mradi wa FAO wa uhakika wa chakula (PESA) katika sekta ya kilimo, mifugo, maendeleo vijijini, uvuvi na kilimo

Si haki kwa watu milioni 690 kulala njaa wakati chakula kinatupwa kila uchao:UN

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Leo ikiwa ni maadhimisho ya kwanza ya siku ya kimataifa ya uelimishaji kuhusu opetevu na utupaji wa chakula, Umoja wa Mataifa umetoa wito hususan kwa nchi za Afrika kuongeza juhudi na kuzichagiza sekta binafsi kuwekeza katika kupunguza upotevu na utupaji wa chakula.

Katika ujumbe maalum wa siku hii shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO limesema upotezvu wa chakula umeongezeka hasa wakati huu wa janga la corona au COVID-19 na linakadiria kwamba katika nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara unasababisha hasara ya dola bilioni 4 kila mwaka. 

Mkurugenzi mkuu msaidizi na mwakilishi wa FAO kanda ya Afrika Abebe Haile-Gabriel amesema, “janga la COVID-19 limekuwa ni kengele ya kutuamsha kutambua haja ya kufanyia mabadiliko mifumo yetu ya chakula na kuifanya iwe na ufanisi na endelevu kwa watu na dunia yetu.”  

Ameongeza kuwa kukabiliana na upotevu na utupaji chakula hususan upunguzaji wa upotevu wa chakula baada ya mavuno barani Afrika ni muhimu katika kufikia lengo la kutokomeza njaa. 

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiongeza sauti yake katika tatizo hilo la upotevu na utupaji wa chakula amesema, “ni kosa la kimaadili katika dunia ambayo ina chakula cha kutosha kulisha watu wote kila mahali, lakini bado watu milioni 690 wanaendelea kulala njaa na wengine bilioni 3 hawawezi kumudu chakula bora.” 

Amesisitiza kwamba changamoto hiyo pia inaathiri maliasili kama maji, udongo na nishati, bila kutaja nguvu na muda wanaotumia binadamu kuzalisha chakula. 

Guterres amesema hofu ya kimataifa ni katika utimizaji wa malengo ya maendeleo endelevu namba 2 la kutokomeza njaa na namba 12 linalotaka kupunguza upotevu na utupaji chakula kwa asilimia 50 ifikapo 2030. Hivyo ametoa wito wa hatua zaidi kuchukuliwa kote duniani ili kufikia malengo hayo. 

Barani Afrika upotevu mkubwa wa chakula hutokea zaidi kati ya muda wa mavuno na mauzo ni kiasi kidogo sana hupotezwa na watumiaji baada ya kununua chakula hicho. 

Miongoni mwa sababu kubwa zinazochangia upotevu wa chakula Afrika ni ukosefu wa mfumo wa baridi wa kuhifadhi vyakula hasa vinavyoharibika haraka, uhaba wa maghala ya kuhifadhia chakula kwa muda mrefu na ujuzi mdogo wa mchakato wa usindikaji vyakula miongoni mwa jamii za wakulima wadogowadogo.