Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatutawatupa raia wa Sudan Kusini-UNMISS 

Familia iliyotawanywa ikiondoka katika kambi ya ulinzi wa raia ya Umoja wa Mataifa mjini Juba kurejea nyumbani kwao Jonglei Sudan Kusini
UN Photo/Isaac Billy
Familia iliyotawanywa ikiondoka katika kambi ya ulinzi wa raia ya Umoja wa Mataifa mjini Juba kurejea nyumbani kwao Jonglei Sudan Kusini

Hatutawatupa raia wa Sudan Kusini-UNMISS 

Wahamiaji na Wakimbizi

Nchini Sudan Kusini, mchakato wa kuzibadili zilizokuwa kambi za ulinzi wa raia chini ya mpnago wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini, UNMISS kuwa kambi za wakimbi wa ndani unaendelea. 

Ni katika eneo la Bor nchini Sudan Kusini katika kambi ya ulinzi wa raia iliyokuwa chini ya UNMISS lakini sasa makubaliano kati ya mamlaka za Jonglei na UNMISS tayari yametiwa saini kuzitaka mamlaka za serikali kuwahakikishia wakazi wapatao 1900 kuwa hakuna hata mmoja wao atakayelazimishwa kuondoka kambini humo. 

Mahema yametapakaa katika eneo hili ambayo ni makazi ya Diu Billiu Majok na familia zingine nyingi zilizokimbia makazi yao wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe mnamo mwaka 2013. Yeye na ndugu zake wengine wanne wamesalia katika kambi ya ulinzi wa raia ya Umoja wa Mataifa iliyoko Bor kwa miaka 7 wakati watoto wake wametawanyika katika mji wao wa nyumbani wa Fangak unaopakana  na Uganda.  

Matumaini ya Majok ni kuwa familia yake iliyotawanyika itaungana tena na anaona kuwa mabadiliko haya ya kutoka kambi ya ulinzi wa raia kuwa kambi ya wakimbizi wa ndani ni ishara chanya kuelekea kwenye amani,“niko tayari kuondoka katika kambi wakati wana usalama watakapokuwa tayari. Kisha nitaondoka haraka hata kama sina nyumba huko nje. Serikali itaniweka mahali wanapoweka wakimbizi wa ndani na nitasalia hapo pamoja na wakimbizi wengine wa ndani au popote serikali itakaponiweka.” 

Kambi hii ni ya kwanza chini ya ulinzi wa Umoja wa Mataifa kubadilishwa kuwa kambi ya wakimbizi wa ndani chini ya usimamizi wa serikali ya Sudsan Kusini.  

UNMISS taratibu inaondoa vikosi vyake kulingana na hali inavyotengamaa. Hii inasaidia walinda amani kuweza kwenda kusaidi katika maeneo mengine yenye hali tete. Kanali Errington Kojo Commey wa UNMISS anasema,"kitu pekee ambacho kimebadilika ni kuondolewa kwa walinzi kutoka mahali hapa. Tutaendelea kuwashirikisha. Tumeongeza idadi ya doria zinazokuja hapa kwa hivyo uwepo wetu ni wa milele. Uwepo wetu uko kambini kila wakati. Tuko hapa. Sio kama tumelala au tumewatelekeza." 

UNMISS itaendelea kusaidia wakati inapohitajika kama sehemu ya jukumu lake la  kulinda haki za raia kote nchini.