Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita, mabadiliko ya tabianchi na COVID-19 vyatishia hatma ya wanawake na watoto:UN 

Wanawake na wasichana wakibeba maji huko Nigeria
World Bank
Wanawake na wasichana wakibeba maji huko Nigeria

Vita, mabadiliko ya tabianchi na COVID-19 vyatishia hatma ya wanawake na watoto:UN 

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Hatua zilizopigwa ili kuboresha afya ya wanawake na Watoto ziko njiapanda kutokana na tishio la vita, mabadiliko ya tabianchi na janga la corona au COVID-19 kwa mujibu wa ripoti mpya ya mkakati wa kila mwanamke, kila mtoto iliyotolewa leo na Umoja wa Mataifa. 

Ripoti hiyo “kulinda hatua zilizopigwa, ukuaji, mtazamo mpya na kujikwamua”  imeainisha kwamba tangu kuzinduliwa kwa mkakati huo miaka 10 iliyopita ukiongozwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuna hatua kubwa ambazo zimepigwa katika kuimarisha afya ya wanawake, watoto na vijana barubaru kote duniani. 

Kwa mfano vifo vya watoto wa chini ya miaka mitano vilifikia kiwango cha chini kabisa mwaka 2019 na watoto zaidi ya milioni moja wamepewa chanjo katika muongo mmoja uliopita. 

Ripoti imeongeza kuwa kiwango cha utoaji chanjo, wahudumu wenye ujuzi na fursa ya upatikanaji maji salama ya kunywa kimefikia asilimia 80. 

Vifo vya kina mama vimepungua kwa asilimia 35 tangu mwaka 2000  huku punguzo kubwa likishuhudiwa kuanzia mwaka 2010 na inakadiriwa kwamba ndoa za utotoni milioni 25 zimeepukwa katika muongo mmoja uliopita. 

Changamoto iliyopo 

Hata hivyo ripoti hiyo imesema vita, changamoto ya mabadiliko ya tabianchi na janga la corona au COVID-19 vinatishia afya na ustawi wa Watoto na barubaru. 

Hususan janga la COVID-19 linaongeza pengo la usawa lililopo huku kukiarifiwa usumbufu mkubwa katika huduma za msingi za afya na hivyo kuathiri wale walio hatarini hususan wanawake na watoto. 

Wakati wa hatua za watu kusalia majumbani kutokana na janga la COVID-19, shule zilifungwa katika nchi 192 na hivyo kuathiri jumla ya wanafunzi bilioni 1.6.  

Ukatili majumbani na ukatili wa wasichana na wanawake umeongezeka na wakati huohuo uamasikini na njaa navyo vinaongezeka. 

“Hata kabla ya janga la COVID-19 mtoto wa chini ya umri wa miaka 5 alikuwa anakufa kila baada ya sekunde sita duniani” amesema mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na kuongeza kwamba “mamilioni ya Watoto wanaishi kwenye maeneo yenye vita na hali hiyo tete imeongezeka Zaidi tangu kuzuka kwa janga la corona. Lazima tushirikiano kwa Pamoja kukidhi mahitaji ya dharura yaliyosababishwa na janga hili huku tukiimarisha mifumo ya afya. Na hadi hapo itakavyofanyika hivyo ndio tutaweza kulinda na kuokoa maisha.” 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo mwaka 2019 watoto milioni 5.2 wenye umri wa chini ya miaka mitano na barubaru milioni moja walipoteza Maisha kutokana na sababu zinazoweza kuzuilika. 

Kila sekunde 13 mtoto mchanga anapoteza Maisha, kila saa wanawake 33 walipoteza Maisha wakati wanajifungua na wasichana 33,000 kwa siku walishinikizwa kuingia katika ndoa na mara nyingi kwa wanaume ambao ni wakubwa sana kwao. 

Mizizi iliyokita ya pengo la usawa 

Ripoti pia imetathimini mizizi iliyokita ya pengo la usawa ambao unaendelea kuwanyima wanawake, watoto na barubaru haki zao na kueleza kwamba mahali mtoto alipozalia ni chachu ya kuishi kwake. 

Ripoti hiyo inasema mwaka 2019 asilimia 82 ya vifo vya Watoto wa chini ya umri wa miaka 5 na asilimia 86 ya vifo bvya kina mama vilitokea Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na Asia Kusini. 

Maambukizi 9 kati ya 10 ya HIV kwa watoto yalifanyika Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara. Na vifo vya Watoto wachanga, kina mama, Watoto wa chini ya miaka 5 na barubaru vilikuwa juu sana katika nchi zilizoathirika na vita. 

“Kwa muda mrefu suala la afya na haki za wanawake , Watoto na vijana barubaru halijapewa uzito unaostahili na huduma zimekuwa hazitoshelezi wala kufadhiliwa vya kutosha,” amesema Helen Clack waziri mkuu wa zamani wa New Zealand na mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa ushirikiano wa afya ya mama, Watoto na Watoto wachanga. 

Ameongeza kuwa “Natoa wito kwa wadau wote kufanyakazi Pamoja kusaidia serikali kuimarisha mifumo ya afya na kushughulikia changamoto ya pengo la usawa ambalo linazuia kupiga hatua.” 

Ripoti imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kipambana na COVID-19 huku ikienzi na kutimiza ahadi zake ambazo zitaboresha maisha ya wanawake na watoto na sio kuongeza pengo baina ya ahadi na hali halisi. 

Imesema hatua zilizopigwa katika muongo uliopita lazima zilindwe  dhidi ya athari za janga la COVID-19. 

Imesisitiza kwamba bila juhudi kubwa za kuzuia vifo vya watoto , Watoto milioni 48 wa chini ya miaka 5 wanaweza kufa kati ya mwaka 2020 na 2030 na karibu ya nusu ya hivyo hivyo vitakuwa vya Watoto wachanga. 

Kuwekeza katika afya 

Ripoti imetoa wito kwa nchi kuendelea kuwekeza katika afya ya wanawake, Watoto na barubaru katika nyanja zote. 

“Wakati tunakabiliana na janga la COVID-19 na kuandaa mustakabali bora wenye amani ya kudumu, ikiwemo majumbani, ni lazima tuseme wazi kwamba haki za wanawake na wasichana si suala la mjadala. Hata katika wakati wa migogoro na hususani wakati wa migogoro afya yao ya uzazi na haki zao lazima zilindwe kwa gharama yoyote ile” amesema Natalia Kanem mkurugenzi mtendani wa shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani UNFPA

Ripoti hiyo imekumbusha kwamba mkakati wa kila mwanamke, kila mtoto ni muhimu sasa kuliko wakati mwingine wowote hasa tukiingia katika muongo wa mwisho wah atua kwa ajili ya ,maendeleo endelevu SDGs ikiwa ni katikati ya janga la kimataifa la kiafya. 

Lazima kuendelea kuchagiza hatua katika sekta zote kupata uwekezaji unaohitajika na kulinda hatua zilizopigwa . 

Nasye mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema “Hakuna sahaka kwamba janga la COVID-19 limechjelewesha juhudi za dunia za kuboresha afya na ustawi wa wanawake na Watoto, lakini hili litumike tu kutuimarisha katika dhamira yetu. Na sasa turejee ahadi yetu ya kuhakikisha tuna afya, usalama, haki na dunia endelevu kwa wanawake, Watoto na vizazi vijavyo.