Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wapalestina wasubiri hadi lini kupata suluhu yenye haki?-Mahmoud Abbas

Rais Mahmoud Abbas wa Taifa la Palestina akihutubia mjadala Mkuu wa Baraza la Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA75 kwa njia ya video.
UN Photo/Eskinder Debebe)
Rais Mahmoud Abbas wa Taifa la Palestina akihutubia mjadala Mkuu wa Baraza la Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA75 kwa njia ya video.

Wapalestina wasubiri hadi lini kupata suluhu yenye haki?-Mahmoud Abbas

Amani na Usalama

Rais wa Palestina Mahmoud Abbas amehoji kwa viongozi wa dunia kwenye mjadala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kikao cha 75 unaoendelea leo Ijumaa mjini New York Marekani na kwa kupitia mtandao kuwa watu wake wanapaswa kusubiri mpaka lini ili kuweza kupata suluhu yenye haki? .

Rais Abbas ameweka bayana madhila na zahma wanayopitia watu wa Palestina kila siku wakati dunia ikiangalia bila kuchukua hatua. 

“Ni kwa muda gani tunapaswa kungoja hadi kupatikana kwa suluhisho la haki kwa suala la Palestina, suluhu ambayo itahakikishwa na sheria za kimataifa?  

Abbas amewauliza viongozi hao ambao kwa asilimia kubwa wanashiriki mjadala wa Baraza kuu kwa kupitia mtandao. 

Akiongeza maswali kwa nchi wanachama hao wa Umoja wa Mataifa kiongozi huyo wa Wapalestina amehoji, "ni kwa muda gani raia wa Palestina wataendelea kuishi wakikaliwa na Israel, tutasubiri hadi lini ili kupata jawabu la haki yetu na suluhu kwa hali ya mamilioni ya wakimbizi wa Palestina?” 

Rais Abbas ameongeza kuwa watu wa Palestina wameishi katika ardhi waliyorithi kwa mababu zao kwa miaka 6,000 na kuongeza kuwa wataendelea kusalia katika ardhi hiyo na kupambana na kitendo cha kukaliwa na Israel, unyanyasaji unaofanywa na Israel na kusalitiwa hadi pale watakapopata haki yao. 

“Licha ya changamoto na vikwazo vyote , hatutoungama, hatutosalimu amri na hatutoafiki hatua yoyote inayowanyima haki Wapalestina.” Amesisitiza kiongozi huyo na kuahidi kwamba watashinda. 

Rais huyo wa Palestina amesisitiza na kuisihi jumuiya ya kimataifa kwamba ina wajibu mkubwa wa kuhakikisha suluhu ya amani ya kudumu kwa suala la  Mashariki ya Kati inapatikana na kwa mtazamo wake suluhu pekee ni kuwa na mataifa mawili la Palestina na Israel ambayo yataishi kwa amani pamoja, suluhu ambayo pia ndiyo inayopigiwa upatu na Umoja wa Mataifa. 

TAGS: Plestina, UNGA75, Mashariki ya Kati, amani, Mahmoud Abbas