Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tumechoka kukimbia tunaomba msaada: wakimbizi waathirika wa mafuriko Sudan 

Moja ya maeneo yaliyokumbwa na mafuriko jimboni Khartoum nchini Sudan
UNOCHA
Moja ya maeneo yaliyokumbwa na mafuriko jimboni Khartoum nchini Sudan

Tumechoka kukimbia tunaomba msaada: wakimbizi waathirika wa mafuriko Sudan 

Msaada wa Kibinadamu

Wakimbizi, wakimbizi wa ndani na jamii zinazohifadhi wakimbizi nchini Sudan wameathirika vibaya na mafuriko makubwa yanayoendelea nchini humo na sasa wanahitaji msaada kwani wanasema wamechoka kukimbia, kwa mujibu shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR. 

Katika viunga vya mji mkuu wa Sudan Khartoum, kutana na mkimbizi Bak mwenye umri wa miaka 80 kutoka Sudan Kusini akijaribu kukusanya vipande vya mabati vilivyosalia baada ya kibanda chake kusambaratishwa kabisa na mafuriko kufuatia mvua kubwa iliyonyesha mfululizo kwa juma zima. Bak anasema,“kwa siku saba maji yalizingira banda langu kila mahali, hapa ndipo ninapolala, sikuweza kukimbia kwa sababu sikutaka kuacha vitu vyangu. Nahitaji msaada wa malazi na nguo.” 

Hivi sasa shirika la UNHCR na wadau wengine likiwemo shirika la save the children na shirika lisilo la kiserikali la msaada wa majanga Sudan ADD, wanagawa msaada wa vifaa visivyo chakula kwa watu 170,000 wakiwemo wakimbizi, wakimbizi wa ndani na jamii zinazowahifadhi. 

Hata hivyo inakadiriwa kwamba takribani watu 800,000 wameathirika na mafuriko hayo, huku nyumba nyingi, vituo vya maji na vyoo nchi nzima ama vimeharibiwa vibaya au kusambaratishwa kabisa. 

Wakimbizi wametajwa kuwa waathirika wakumbwa  wa mafuriko haya, kama ilivyo kwa Bak, Christina Diang naye ni mkimbizi kutoka Sudan Kusini hema lake sasa linavuja baada ya kuharibiwa na mvua hizo  na hajui la kufanya,“sitaki kuondoka nataka kuendelea kuishi kwenye nyumba yangu, kuboresha hali ya maisha na kupeleka watoto wangu shule.” 

Kwa sasa UNHCR inasema msaada zaidi na wa haraka wa kibinadamu unahitajika lakini shirika hilo linakabiliwa na ukata wa ufadhili kwani hadi kufikia katikati ya mwezi huu wa Septemba limepokea asilimia 38 tu  ya dola milioni 274.9 zinazohitajika kuisaidia Sudan kwa mwaka huu wa 2020.