Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua tulizochukua dhidi ya COVID-19 zimedhihirishia ulimwengu uthabiti wetu Afrika 

Mwanafunzi wa kike nchini Ghana akinawa mikono kwa sabuni kabla ya kurejea darasani ikiwa ni sehemu ya mpango wa serikali kuhakikisha elimu inaendelea huku wakidhibiti maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.
UNICEF/Geoffrey Buta

Afya

Fikra za baadhi ya watu kuwa maelfu kwa maelfu ya watu barani Afrika watapukutika kutokana na janga la ugonjwa wa Corona, au COVID-19 zimekuwa ndivyo sivyo baada ya bara hilo kuchukua hatua kitaifa na kikanda na hatimaye hadi sasa kudhihirisha umuhimu wa mshikamano katika kukabili adui. Hilo limebainishwa wakati wa hotuba za marais waliohutubia mjadala mkuu wa mkutaon wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa njia ya mtandao kutokana na vikwazo vilivyopo Marekani kutokana na janga la Corona. Flora Nducha anamleta Assumpta Massoi ambaye amefuatilia hotuba za viongozi hao na anaeleza kwa kina.

Naanza na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambayo ujio wa Corona ulikuwa ni sawa na kuongeza chumvi kwenye kidonda kutokana na taifa hilo kugubikwa siyo tu na mapigano mashariki mwa nchi hiyo, bali pia gonjwa la Ebola. Hata hivyo katika hotuba yake, Rais Felix Tshisekedi amesema kwa kupitia  ushirikiano wa kimataifa wameweza kudhibiti maambukizi mapya kwa kuwa, “mgonjwa wa kwanza wa Corona alipobainika jijini Kinshasa tarehe 10 mwezi Machi mwaka 2020, tulitangaza kuwa ni janga la kiafya la umma nchini lakini baada ya kuunda kikosi kazi cha kiserikali. Hata hivyo uzoefu wetu wa kukabiliana na Ebola umetusaidia kudhibiti ugonjwa huo.” 

Rais wa DRC Félix Tshisekedi  akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 75 wa  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa njia ya video kutoka Kinshasa.
UN WebTV
Rais wa DRC Félix Tshisekedi akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa njia ya video kutoka Kinshasa.

Kwa upande wa Kenya, Rais Uhuru Kenyatta ametambua madhara ya COVID-19 ikiwemo kusababisha ongezeko la ukatili wa kijinsia lakini akaenda mbali zaidi kuzungumzia kibara walipitisha mkakati wa wa kupunguza COVID-19 ambao umekuwa na mafanikio makubwa na kwamba, “kile ambacho tumejifunza katika miezi sita iliyopita, hakuna nchi na narudia, hakuna nchi inayoweza kushughulikia janga la kiwango hiki, peke yake. Imetubidi kufanya kazi kwa pamoja ili kurejea katika hali nzuri.” 

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA75 kwa njia ya video.
UN Photo/Evan Schneider
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA75 kwa njia ya video.

Rais Paul Kagame wa Rwanda ametumia hotuba yake akisema kuwa ingawa COVID-19 siyo tu imesababisha vifo bali pia imesukuma watu wengi zaidi katika ugumu usiotarajiwa lakini kwa vyovyote vile, "tutashinda jaribio hili, kwani tunazo zana za kutamalaki katika afya, usawa wa kijinsia, mazingira, maendeleo endelevu, ujumuishaji wa kidijitali, na haki ya rangi zote. Inahusu maadili mazuri tunayowekeza katika taasisi zetu.” 

Rais Paul Kagame wa Jamhuri ya Rwanda akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA75 kwa njia ya video.
UN Photo/Evan Schneider
Rais Paul Kagame wa Jamhuri ya Rwanda akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA75 kwa njia ya video.

Kwa Burundi gonjwa la Corona nalo lilitikisa taifa hilo ambapo Rais Evariste Ndayishimiye ambaye alichaguliwa katikati ya janga hilo amesema, janga hili halichagui mtu yeyote linapoambukiza na ndio maana, “limeonesha umuhimu ushirikiano wa kimataifa na mshikamano wa jinsi tunavyoshughulikia majanga na mizozo duniani.” 

Rais Evariste Ndayishimiye akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA75 kwa njia ya video.
UN Photo/Eskinder Debebe)
Rais Evariste Ndayishimiye akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA75 kwa njia ya video.

Rais mwingine aliyechaguliwa katikati ya janga la Corona ni Rais Lazarus Chakwera wa Malawi,  ambaye amechukua madaraka mwezi Juni mwaka wa huu wa 2020 . Yeye amekiri kuwa uchumi wa Malawi umetikiswa kutokana na sababu lukuki ikiwemo kutokuuunganishwa na bahari, lakini mweleko sasa ni jinsi ya kukwamuka. 

Rais Lazarus chakwera wa Malawi (kwenye skrini) akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA75 kwa njia ya video kutoka Malawi.
UN/Eskinder Debebe
Rais Lazarus chakwera wa Malawi (kwenye skrini) akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA75 kwa njia ya video kutoka Malawi.

Akiwa mwenyekiti wa kundi la nchi zinazoendelea, LDCs, amesema kwa mwelekeo wa sasa kuna hatari kubwa ya nchi hizo kushindwa kulipa madeni kwa hiyo, "tunatambua uamuzi wa Benki ya Dunia, shirika la fedha duniani, IFM na shirika la maendeleo ya ushirikiano wa kiuchumi, OECD na wadau wengine wengi wa kusitisha kwa muda ulipaji madeni kwa LDCs. Lakini kwa kutambua jinsi janga hili litaendelea kuwepo kwa muda mrefu na madhara yake zaidi, tunaomba na tunatumaini kufutwa kabisa kwa madeni, na pia kuongezwa muda wa sitisho la kulipa madeni.”