Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni wakati wa kuwatambua mabaharia na wahudumu wengine wa meli kama wafanyakazi muhimu:UN

Meli ya mizigo ikipakua makasha ya mizigo bandarini
IMO
Meli ya mizigo ikipakua makasha ya mizigo bandarini

Ni wakati wa kuwatambua mabaharia na wahudumu wengine wa meli kama wafanyakazi muhimu:UN

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa viongozi kote duniani kuwatambua mabaharia na wafanyakazi wengine wa melini kuwa ni wafanyakazi muhimu kutokana na mchango wao hasa wakati huu wa janga la corona au COVID-19.

Katika ujumbe wake wa siku ya usafiri wa bahari duniani hii leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema janga la COVID-19 limedhihirisha kazi kubwa na kujitolea kunakofanywa na mabaharia 2 ambao wanaohudumia dunia kupitia usafiri wa meli. 

Kaulimbiu ya mwaka huu ya siku hiyo ni “usafirishaji endelevu kwa ajili ya sayari endelevu” ikizingatia kwamba usafiri wa meli umeendelea kusafirisha zaidi ya asilimia 80 ya biashara duniani ikiwemo vifaa muhimu vya kitabibu, chakula na bidhaa zingine za msingi ambazo ni muhimu kwa ajili ya kupambana na kujikwamua na COVID-19. 

Guterres ameongeza kwamba “Bado nina hofu kubwa kuhusu ongezeko la mgogoro wa kibinadamu na kiusalama unaowakabili maelfu ya wafanyakazi hawa muhimu. Licha ya changamoto kubwa zilizoletwa na janga la COVID-19, mabaharia wameendelea bila kuchoka kusaidia katika mnyororo wa kiufundi wa usafirishaji.” 

Amemesema wafanyakzi hao wakiwa wamechoka kiakili na kimwili, wakiwa mbali na familia zao na wapendwa wao, muda wanaoutumia baharini sasa umeongezeka zaidi ya inavyotakiwa kwenye mikataba ya kimataifa huku wengine wakilazimika kuwa safarini kwa zaidi ya miezi 17. 

Guterres ameonya kwamba hali hiyo hususan kwa mabaharia waliochoka kupindukia haiwezi kuendelea bila ukomo na athari zake katika usafirishaji wa meli wa kimataifa zitakuwa mbaya. 

Kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu ametoa rai ”Narejea wito wangu wa serikali kushughulikia changamoto hii kwa kuwatangaza rasmi mabaharia na wafanyakazi wengine wa melini kama wafanyakazi muhimu, kuhakikisha mnawabadilisha kwa usalama wafanyakazi hao na kutekeleza mikataba iliyiopitishwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa, kitengo cha kimataifa cha usafirishaji wa bahari na  shirikisho la kimataifa la wafanyakazi wa sekta ya usafirishaji, ili kuruhusu mabaharia waliokwama kusafirishwa kwenda makwao na wafanyakazi wengine kuchukua nafasi zao.” 

Akiunga mkono hilo Katibu Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la usafiri wa bahari IMO Kitack Lim amesema katika kujikwamua na janga la COVID-19 mabaharia, wafanyakazi wengine wa melini na sekta nzima ya usafirishaji kwa njia ya bahari vitakuwa na jukumu kubwa sana.

Amesisitiza kwamba kwa malengo ya muda mrefu sekta hiyo pia itakuwa na jukumu kubwa katika kutimiza kama sio yote basi asilimia kubwa ya malengo ya mamendeleo endelevu SDGs . 

Shirika la IMO limeweka viwango vya kimataifa ambavyo vinasaidia usafirishaji salama na unaozingatia mazingira. 

Umoja wa Mataifa umesisitiza kwamba sekta ya usafiri wa bahari inashikilia biashara ya dunia na itaendelea kuwa muhimu katika kujenga mustakabali endelevu kwa ajili ya wat una sayari dunia.  Siku ya usafiri wa bahari duniani huadhimishwa kila mwaka Septemba 24.