Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN iko tayari kuyasaidia mataifa yasiyo na bahari, kujikwamua na COVID-19 

Kontena zikiwa bandarini jamhuri ya São Tomé and Príncipe zikisubiri kusafirishwa
UNCTAD/Jan Hoffmann
Kontena zikiwa bandarini jamhuri ya São Tomé and Príncipe zikisubiri kusafirishwa

UN iko tayari kuyasaidia mataifa yasiyo na bahari, kujikwamua na COVID-19 

Ukuaji wa Kiuchumi

Mfumo wa umoja wa Mataifa umesema unashikamana na mataifa yanayoendelea yasiyo na bahari ambayo yanakosa fursa muhimu za viunganishi vya biashara na kuyasaidia katika juhudi zao za kujijenga upya pindi janga la corona au COVID-19 litakapokwisha. 

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo akizungumza kwa njia ya video kwenye mkutano wa ngazi ya juu wa mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi hizo. Bwana Guterres amesema kwamba zaidi ya changamoto ambazo zinajumuisha uingiliaji mkubwa na uvurugaji wa biashara, usajiri na usambazaji, hatari ya changamoto ya madeni nayo inanyemelea. 

“Kutokana na athari za COVID-19 madeni duniani yameongezeka kwa kiwango kisicho cha kawaida, na katika baadhi ya nchi zilizo hatarini zaidi ya robo ya makusanyo ya umma yametumika kulipia madeni na hivyo kuathiri sana uwezo wa kifedha.” 

Changamoto kubwa sio tu kwamba zinatishia ukuaji wa uchumi na maisha bali pia zinaathiri uwezo wa mataifa hayo kutekeleza ajenda ya 2030 ya maendfeleo endelevu na mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi, ameongeza bwana Guterres. 

Ushirika kwa ajili ya suluhu 

Licha ya changamoto zote hizo Katibu Mkuu amesema, “Umoja wa Mataifa uko hapa kwa ajili ya kushirikiana nayi kuhusu suluhu.” 

Suluhu hizo zinajumuisha upunguzaji wa hewa chafuzi, miundombinu na usafiri salama, kukusanya fedha kutoka kwa wafadhili wa serikali na binafsi kuepuka kuwa tegemezi wa uchumi unaotegemea mafuta kisukuku na kuingia katika mifumo ya nishati jadidifu na kupambana na uingizaji haramu wa fedha. 

Bwana Guterres amesisitiza kuwa, “tunahitaji kuhakikisha kwamba rasilimali na msamaha wa madeni vinazifikia nchi zote zinazohitaji rasilimali hizo ili kutoa upenyo wa fursa za uwekezaji katika kujikwamua na kutimiza malengo ya maendeleo endelevu SDGs." 

Pamoja ya hayo ameongeza kuwa uwezekano wa biashara katika nchi zisizo na bahari lazima uongezwe na ushirikiano baina ya nchi zinazoendelea zisizo na bahari na zile wanakopitishia bidhaa zao lazima uimarishwe. 

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema mkutano wa viongozi wa masuala ya fedha kwa ajili ya maendeleo wakati huu wa COVID-19 na zaidi utakaofanyika Jumanne ijayo utasaidia kuchagiza dhamira hiyo na hatua za kuchukuliwa. 

Bwana Guterres pia ametoa wito kwa nchi za mataifa yasiyo na bahari kutekeleza vipengele sita muhimu kwa ajili ya kuzingatia mabadiliko ya tabianchi wakati wa kujikwamua kiuchumi ambavyo ni  Mosi kuwekeza katika sekta ya ajira zinazojali mazingira, kutofadhili sekta zinazochafua mazingira, kukomesha ruzuku kwa mafuta kisukuku, kuwajibika kwa hatari na fursa kwa ajili ya mabadiliko ya tabianchi katika sera zote na maamuzi ya kifedha, kufanyakazi kwa Pamoja na kutomuacha yeyote nyuma. 

Guterres amezihakikishia nchi hizo kwamba, “mfumo wa Umoja wa Mataifa utaendelea kuwasaidia katika juhudi zenu za kutimiza malengo jumuishi ya maendeleo endelevu kwa ajili ya watu wenu wakati huu mkipambana na hatimaye kujikwamua kutoka katika mgogoro wa COVID-19.”