Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zama za kidijitali zadhihirisha ongezeko la pengo la usawa duniani: UN 

Wasichana barubaru wakitumia simu ya mkononi nje ya maabara ya teknolojia katika jimbo la Damietta, Misri.
© UNICEF/Shehzad Noorani
Wasichana barubaru wakitumia simu ya mkononi nje ya maabara ya teknolojia katika jimbo la Damietta, Misri.

Zama za kidijitali zadhihirisha ongezeko la pengo la usawa duniani: UN 

Utamaduni na Elimu

Tofauti za kidijitali linadhihirisha pengo la usawa lililopo katika masuala ya kijamii, kitamaduni na kiuchumi amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. 

Akizungumza kwa njia ya video kwenye mkutano wa ngazi ya juu wa ushirikiano wa kidijitali unaofanyika kandoni mwa mjadala wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa hii leo Antonio Guterres amesema mfano katika nchi 2 kati ya 3 wanaume wanaotumia mtandao wa intaneti ni wengi kuliko wanawake. 

Na haya yamebainika zaidi wakati huu wa janga la corona au COVID-19 pamoja na kuweka bayana changamoto zingine za kidijitali. 

Pengo la usawa 

Katika mkutano huo wa ngazi ya juu uliohudhuriwa pia na makampuni makubwa ya masuala ya kidijitali kama Microsoft, Google na Facebook na wahusika wa masuala ya mtandao kama Ali Baba 

Guterres amesema miongoni mwa wasio na fursa za teknolojia za kidijitali sio tu wanawake ambao ni waathirika wakubwa bali pia makundi mengine kama vile wahamiaji, wakimbizi, wazee, vijana, Watoto, watu wenye ulemavu, watu wa vijijini na watu wa asili. 

Lazima tujiulize tunataka kuuona vipi mustakabali ambao watotom wetu wataishi? Je watarithi teknolojia kutoka kwetu ambayo ni ya matajiri peke yao na jamii zinazomudu kuunganishwa na kuacha wengine wote waliosalia duniani duniani nyuma?, au tutahakikisha kwamba vizazi vijavyo vinaweza kutumia teknolojia kuimarisha haki za binadamu, kusak amani na kuboresha Maisha ya watu ikiwemo walio hatarini zaidi?. 

Teknolojia ya kidijitali na janga la COVID-19 

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa katika zama hizi za janga la corona au COVID-19 haja ya kuziba pengo hili la usawa katika dijitali ni laharaka zaidi. 

Nyenzo za kidijitali zimekuwa mkombozi wa maisha kwa mamilioni ya watu compyuta zimekuwa zikitathimini maelfu ya michanganyo ya madawa ili kubaini uwezekano wa dawa na chanjo ya COVID-19. 

Majukwaa ya masoko mtandaoni yamekuwa yakiuza bidhaa muhimu za nyumbani na vifaa tiba, huku majukwaa ya mawasiliano kwa njia ya video yamewezesha elimu na shughuli za kiuchumi kuendelea. 

Wakati huohuo ameongeza kuwa janga la COVID-19 limeongeza matatizo na ugumu Zaidi wa fursa na matumizi ya teknolojia ya kidijitali. 

“Sote tunatambua kwamba kupata takwimu na taarifa sahihi kuhusu maambukizi ya corona ni muhimu katika kupambana na gonjwa hilo na mitandao ya kijamii ina jukumu muhimu hapa, lakini pia imekuwa jinamizi na chanzo cha taarifa potofu na za hatari na pia kuchochea ubaguzi, chuki dhidi ya wageni na ubaguzi wa rangi.” 

Ameongeza kuwa mashambulizi ya kimatandao dhidi ya shirika la afya duniani, hospitali na maabara, vinatishia Maisha ya wat una kuingilia vita dhidi ya gonjwa hilo. 

Amesema pia nyenzo zinazotumika kubaini watu walioambukizwa ili kupambana na kuzia kusambaa kwa virusi wakati huohuo zinatumika kukiuka misingi ya faragha na haki za watu. 

Amekumbusha kwamba wakati teknolojia ya kidijitali inawaruhusu watu katika nchi zenye huduma kubwa ya intaneti kufanyiakazi na kuysoma nyumbani , fursa hii haipatikani kwa kila mtu, kwani watu wengine inabidi wawepo kimwili kazini huku wengine wakipoteza ajira zao au kutopata fursa za teknolojia ya intaneti au siumu za rununu, na hili linatia hofiu kubwa hasa kwa watu masikini na jamii zilizo hatarini zaidi. 

Mwelekeo wa ushirikiano wa kidijitali 

Mwezi Juni mwaka huu Katibu Mkuu aliwasilisha mtazamo wa ushirikiano wa kidijitali. 

Wakati wa kuandaa mtazamo huo Umoja wa Mataifa ulitegemea mapendekezo ya jopo la ngazi ya juu kuhusu ushirikiano wa kidijitali ambalo aliliunda mwaka 2018 likiongozwa na Melinda Gates and Jack Ma. 

Umoja wa Mataifa unang’ang’ana kuhakikisha kwamba ifikapo mwaka 2030 kila makazi ya mtu mzima duniani yana fursa za mitandao ya kidijitali Pamoja na huduma za fedha na afya kwenye mitandao ya intaneti, na kwenye majukwaa ya kidijitali ikiwemo mitandao ya kijamii na wakati huohuo haki za binadamu zikiheshimiwa. 

Guterres amesema “Hatuwezi kujua athari za kijamii za janga la corona zitakavyokuwa baada ya janga hilo, lakini kitu kimoja kilicho bayan ani kwamba teknolojia za kidijitali zitakuwa muhimu zaidi katika mchakato wa kujikwamua na janga hilo kuliko wakati mwingine wowote.Na hii inamaanisha kwamba wale ambao hawatakuwa na fursa ya teknolojia hizo wataendelea kusalia nyuma zaidi na zaidi” 

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa anaamini kwamba binadamu hawataweza kutumia fursa kamilifu ya faida za zama za kidijitali bila kuziba mapengo yaliyopo na kupunguza athari zake. 

Na hilo amesema litawezekana tu endapo juhudi zinafanyika kwa ushirikiano kwenye ngazi ya kimataifa. 

Amehitimisha kwa kusema kwamba “Katika mkakati wangu ninatoa wito kwa mambo matatu ambayo ni mawasiliano, kuheshimu na kulinda. Nitarajia kushirikiana na serikali, asasi za kiraia na sekta vinafsi kusongesha mbele suala hili kwa faida ya watu wote duniani”