Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lugha ya ishara lazima ijumuishwe katika kujikwamua na janga la COVID-19 

Mkalimani wa lugha ya ishara akiwa katika mkutano
Centre/Stéphanie Coutrix
Mkalimani wa lugha ya ishara akiwa katika mkutano

Lugha ya ishara lazima ijumuishwe katika kujikwamua na janga la COVID-19 

Utamaduni na Elimu

Mwaka huu siku ya kimataifa ya lugha ya ishara inaadhimishwa katikati ya janga la corona au COVID-19, janga ambalo limemkumba kila mtu wakiwemo jamii ya viziwi, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. 

Katika ujumbe wake kwa ajili ya siku hii Antonio Guterres ameelezea kutiwa moyo na baadhi ya nchi ambazo zimekuwa zikitoa matangazo kwa umma na taarifa kuhusu COVID-19 kwa kutumia lugha za ishara za kitaifa kuhakikisha jamii hiyo pia haiachwi nyuma. 

Guterres amerejelea wito wake kwamba hatua zote za kupambana na kujikwamua na jnga la COVID-19 ni lazima zitoe fursa kwa wote. 

Mkalimani wa lugha ya ishara wakati wa tukio maalumu la Umoja wa Mataifa.
UN Photo/Manuel Elías
Mkalimani wa lugha ya ishara wakati wa tukio maalumu la Umoja wa Mataifa.

 

Mipango ya wenye ulemavu 

Katibu Mkuu amesema mkakati wa Umoja wa Mataifa wa ujumuishaji wenye ulemavu ambao ulizinduliwa mwaka jana una lengo la kuimarisha juhudi kwa ajili ya ushiriki na ujumuishwaji kamilifu wa watu wenye ulemavu katika kila tunachokifanya  ikiwemo wakati wa migogoro na majanga. 

Amefafanua mkakati huo kwa kuuita kwamba, “ndio njia pekee ya kutimiza ahadi ya agenda ya maendeleo ya 2030 kwa kutomuacha yeyote nyuma.” 

Ameongeza kuwa, “katika siku hii ya kimataifa ya lugha ya ishara natoa wito kwa viongozi wote wa mashinani, kitaifa na kimataifa kulinda na kuchagiza mchanganyiko wetu wa lugha za ishara na utamaduni ili kila kiziwi aweze kushiriki na kuchangia katika jamii na pia kuweza kufikia uwezo wao.” 

Natoa wito kwa viongozi wote wa mashinani , kitaifa na kimataifa kulinda na kuchagiza tofauti zetu za lugha za ishara na utamaduni-Katibu Mkuu wa UN 

Aina 300 za lugha za ishara 

Kwa mujibu wa shirikisho la dunia la viziwi kuna takribani watu milioni 72 kote duniani ambao ni viziwi  na zaidi ya asilimia 80 ya watu hao wanaishi katika nchi zinazoendelea na kwa pamoja wanatumia lugha tofauti za ishara zaidi ya 300. 

Umoja wa Mataifa unashikilia kwamba siku ya kimataifa ya lugha za ishara inatoa fursa ya kipekee ya kusaidia na kulinda utambulisho wa utofauti wa lugha na utamaduni wa watu ambao ni viziwi na watumiaji wengine wa lugha za ishara. 

Lugha za ishara zinatambulika kikamilifu kama lugha za asili na Umoja wa Mataifa umeweka bayana utofauti wake na lugha za kuzungumzwa. 

Pia kuna siku ya lugha za ishara za kimataifa ambazo zinatumiwa na viziwi katika mikutano ya kimataifa na pia wakati wanaposafiri au kwenye mikusanyiko ya kijamii ambayo inatambulika kama aina ya lugha ya ishara ambayo ni rahisi na isiyo na masharti, kwa kifupi ambayo sio rasmi. 

Changamoto za kimataifa 

Mwaka jana shirikisho la kimataifa la viziwi lilitoa changamoto kwa viongozi wa kimataifa kuchagiza matumizi ya lugha za ishara kwa viongozi wa kijamii, kitaifa na kimataifa. 

Na shirikisho hilo limetaka changamoto hiyo ifanyike kwa ushirikiano na jumuiya za viziwi na mashirika yanayoongozwa na viziwi katika kila nchi.