Mafuriko yafurusha maelfu ya wakimbizi Niger:UNHCR

23 Septemba 2020

Wakimbizi 9,000 wameathirika na mafuriko makubwa yanayoendelea nchini Niger tangu mwezi Julai na sasa wengi wanahitaji msaada wa dharura sio tu wa huduma za chakula na afya bali pia malazi baada ya makazi yao kusambaratishwa kabisa na mafuriko hayo, limesema shirika la umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Katika mji mkuu wa Niger Niamey wakimbizi wakiwa kwenye mtumbwi wakielekea kusaka mahala salama pa kujihifadhi baada ya makazi yao kusamkusombwa na mafuriko. Mitaa imejaa maji na wengine wanajaribu kuokoa chochote kilichosalia. 

Kwa mujibu wa UNHCR wengi wamepoteza kila kitu na wanaishi katika hali mbaya wakiwa na chakula kidogo, bila makazi , vifaa vya kujisafi na maji safi na salama. 

Miongoni mwa waathirika hao ni Balkissa Alhousseyni, mkimbizi kutoka Mali Mali ambaye amepoteza makazi yake na sasa anajibanza kwenye kibanda cha msamaria mwema ambacho ni kidogo na imembidi atengana na familia yake, "Hatuna mahali pa kulala, hatuna huduma za usafi na choo, watoto wetu hawana maisha mazuri, hivi sasa wanalala na kuishi katika vyumba vya madarasa ya shule.” 

Ingawa alibahatika kuokoa asilimia kubwa ya mali yake lakini hana pakuweka vitu vyake hivi sasa vinalala nje,“tuko katika hali mbaya, tunahitaji msaada wa chakula, fedha na malazi, tumekuwa katika hali hii kwa muda mrefu na kama wakimbizi tumepoteza matumaini kabisa.” 

UNHCR inasema wakimbizi hawa wako katika hatari kubwa ya kupata magonjwa kama corona au COVID-19, malaria na kipindupindu. 

Shirika hilo na wadau wengine wanawapatia msaada wa dharura lakini wanasema hali huenda ikawa mbaya zaidi kutokana na matarajio ya mvua na mafuriko zaidi, hivyo hatua za haraka zinahitajika ili kulinda maisha ya maelfu ya wakimbizi hao. 

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud