Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tanzania haikuongozwa na mihemuko ya kisiasa katika kukabili COVID-19 – Balozi Gastorn

Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Kennedy Gastorn wakati wa mahojiano na Idhaa ya Umoja wa Mataifa.
UN News/Anold Kayanda
Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Kennedy Gastorn wakati wa mahojiano na Idhaa ya Umoja wa Mataifa.

Tanzania haikuongozwa na mihemuko ya kisiasa katika kukabili COVID-19 – Balozi Gastorn

Afya

Wakati hii leo, wakuu wa nchi na wawakilishi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wanashiriki mkutano wa ngazi ya juu wa UNGA75 wa kujadili jinsi ya kuepusha upotoshaji wa taarifa na usambazaji wa taarifa potofu wakati huu wa janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19, Tanzania imetaja siri ya mafanikio yake katika kudhibiti gonjwa hilo mara baada ya kubainika mwezi Machi mwaka huu. 

Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Kennedy Gastorn akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa amesema,“siri kubwa sana ya mafanikio ni uongozi wa Rais John Magufuli, aliweza kusimamia vizuri sana jambo hili kwa kuweka mikakati na sera zinazoendana na sayansi na siyo tu mikakati inayoendana na mihemuko ya kisiasa na mihemuko ya dunia wakati ule. Nchi nyingi zilijikuta zinachukua maamuzi ambayo kwa kweli hayana uhalisia katika nchi zao kwa sababu tu mihemuko ya kisiasa na mihemuko ya dunia. Kwa hiyo uongozi tuliokuwa nao kwa kweli ulisaidia sana kuepusha majanga makubwa ambayo yangetokana na maamuzi yasiyo na uhalisia ndani ya nchi.” 

Mwakilishi huyo wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa akaenda mbali zaidi akisema kuwa, “uongozi ulichokifanya kikubwa sana kwanza ni kusisitiza miongozo ambayo ni ya shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, na miongozo ya afya ya pale pale ndani ya nchi, kuboresha sekta ya afya katika kuweka mikakati sahihi ya kukabili janga hilo na pia kuwatoa hofu wananchi. Wananchi walikuwa na hofu kubwa sana. Rais Magufuli alikuwa mstari wa mbele kuwatia moyo wananchi na kuwaondoa wasiwasi na kuwaambia kuwa maisha lazima yaendelee lakini pia kuwapa imani. Aliweka nchi mikononi mwa Mungu na kwa kweli wananchi wengi wa Tanzania wana imani katika dini mbalimbali. Lakini siyo tu hilo, Rais Magufuli ni mwanasayansi na ana utalaam wa kufahamu kemikali. Kwa hiyo nafikiri hili lilimsaidia sana katika maamuzi yake ya kuweza kuiokoa Tanzania. Nchi imefunguliwa, hatuna COVID-19 lakini bado tunachukua tahadhari.