Maoni ya wakazi wa dunia kuhusu UN waitakayo! Wengine waona chombo hicho kiko mbali na maisha yao

22 Septemba 2020

Umoja wa Mataifa ukitimiza miaka 75, wakazi wa sayari ya dunia kutoka nchi maskini hadi tajiri, wanawake hadi wanaume, vijana hadi watoto wametoa maoni yao kuhusu Umoja wa Mataifa wautakao, ikiwa ni matokeo ya utafiti uliofanyika kuanzia mwezi Januari mwaka huu kufuatia wito wa Katibu Mkuu Antonio Guterres.
 

Wakazi hao zaidi ya milioni moja kutoka nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa waliulizwa kuhusu matumaini na hofu juu ya mustakabali wao na vipaumbele vyao kwa ushirikiano wa kimataifa hususan Umoja wa Mataifa ufanye nini ili uweze kuleta mabadiliko chanya na endelevu.

Matokeo yalikuwa katika vipengele vitano na yamechapishwa kwenye ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa.

Utafiti unaendelea katika kusaka chanjo na tiba ya virusi vya Corona, COVID-19
UN Photo/Loey Felipe
Utafiti unaendelea katika kusaka chanjo na tiba ya virusi vya Corona, COVID-19

 

1) Huduma bora za msingi

Wakati huu ambapo dunia imegubikwa na janga la COVID-19, haishangazi kuona kwamba kipaumbele cha kwanza kwa watu wengi walioshiriki utafiti huo ni huduma bora za msingi. Katika nchi nyingi bado kuna mazuio ya kutembea na kutochangamana kwa hivyo watu wengi wametaka kuboreshwa kwa huduma za msingi ikiwemo huduma za afya, maji na kujisafi pamoja na elimu. Watu wengi wanaamini kuwa kupata elimu na haki za wanawake zikizingatiwa basi huduma hizo zitakuwa bora. Kutoka Mexico mshiriki mmoja amesema kuwa: “virusi vimechukua ajira, michangamano, elimu na amani. Hofu iko kila pahali na watu wanashindwa kuchukua hatua ipasavyo kukabili hofu hiyo.”

2) Ushirikiano zaidi wa kimataifa

Janga la COVID-19, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, limepigia mstari ushirikiano wa kimataifa ili kutafiti, kuzalisha na kusambaza chanjo kwa maslahi ya mataifa yote, maskini na tajiri. Tayari Umoja wa Mataifa umepatia msisitizo suala hilo na mataifa yanashirikiana kwa maslahi ya pande zote.

Dodoso la utafiti liko kwa lugha 64 ikiwemo lugha ya Kiswahili.

Halikadhalika inaonekana kuwa idadi kubwa ya washiriki wa utafiti huo, takribani asilimia 87 wanaamini kuwa ushiririkiano wa kimataifa ni muhimu ili kukabili changamoto ya janga la COVID-19 na kwamba janga hilo limethibitisha kuwa mshikamano wa kimataifa ni suala la linalotakiwa kutekelezwa haraka.

Miongoni mwa washiriki kutoka Albania amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji wa pamoja kijamii akisema; “Ni muhimu sana mkakati wowote wa kujikwamua uzingatie ubinadamu na utu. Kile tulichojifunza kwenye janga hili ni kwamba hakuna hata mmoja aliye salama hadi kila mtu yu salama.”

Moja ya maeneo yaliyokumbwa na mafuriko jimboni Khartoum nchini Sudan
UNOCHA
Moja ya maeneo yaliyokumbwa na mafuriko jimboni Khartoum nchini Sudan

3) Hatua kwa tabianchi

Kitendo cha binadamu kushindwa kupunguza kasi ya ongezeko la joto duniani, na kuepusha madhara ya mabadiliko ya tabianchi yaliyosababisha uharibifu wa mazingira kimekuwa jambo lililoshika nafasi ya tatu na kuibua wasiwasi miongoni mwa washiriki. Tatizo lingine ni kuongezeka kwa umaskini, ufisadi serikalini, ghasia kwenye jamii na ukosefu wa ajira. 
Kijana mmoja kutoka China yeye anasema kuwa kila mtu ameathiriwa na mabadiliko ya tabianchi; “Kiwango cha sasa cha mabadiliko ya tabianchi duniani kutokana na uchafuzi wa mazingira kimesababisha wat una jamii nzima kuwa katika hatari zaidi.”

4) Umoja wa Mataifa ujihusishe zaidi

Wakitathmini yaliyopita, washiriki 6 kati ya 10 wanaamini kuwa Umoja wa Mataifa umefanya dunia kuwa pahala bora zaidi na asilimia 74 wanasema kuwa Umoja wa Mataifa ni muhimu iwapo changamoto zinazokabili dunia zitashughulikiwa kwa ufanisi. Hata hivyo nusu ya washiriki wa utafiti huo wanasema kuwa bado hawafahamu vya kutosha kuhusu Umoja wa Mataifa na wanaona uko mbali na maisha yao.

Idadi kubwa wamependekeza kuanzishwa kwa baraza la vijana la kushauri maafisa waandamizi wa Umoja wa Mataifa na mmoja wa washiriki kutoka Brazil amependekeza ushiriki zaidi wa Umoja wa Mataifa kikand; “Umoja wa Mataifa unaweza kuchukua hatua kwa kushiriki zaidi katika shughuli za kikanda na kitaifa, kuwekeza katika mustakabali kwa kupatia wahusika uwezo wa kuchochea maendeleo ya kunyanyua wahusika kwenye jamii.”

Angures Buba, mwenye umri wa miaka 14 akitafuta masafa ya matangazo ya elimu ya darasa la 8 kwa njia ya redio. Hapa ni kwenye mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba na masomo anayosubiria kwa hamu ni Sayansi na Kiingereza.
© UNICEF/Helene Sandbu Ryeng
Angures Buba, mwenye umri wa miaka 14 akitafuta masafa ya matangazo ya elimu ya darasa la 8 kwa njia ya redio. Hapa ni kwenye mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba na masomo anayosubiria kwa hamu ni Sayansi na Kiingereza.

 

5) Imani wa siku zijazo

Linapokuja suala la siku zijazo, vijana washiriki wa utafiti huo na wengine wengi kwenye nchi zinazoendelea wanaonekana kuwa na imani kuliko watu wazima au wale wanaoishi kwenye nchi zilizoendelea. Wakazi wa Asia ya Kati na Kusini na wale wa nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara, wana imani zaidi kuliko wale walioko nchi za Ulaya na Amerika Kaskazini.  “Hakuna asiye na uwezo.” Amesema mwanafunzi mwenye umri wa miaka 17 kutoka shule ya sekondari ya juu nchini Japan.

Utafiti

Utafiti huo wa dakika moja ulifanyika kupitia wavuti (www.un75.online) ulileta kupata maoni ya watu wengi kwa kadri iwezekanavyo na hadi sasa dodoso husika bado liko mtandaoni katika lugha 64 ikiwemo lugha ya Kiswahili.
•    Ili kuhakikisha kuwa wale wasio na mtandao wanaweza kupaza sauti zao, dodoso lilisambazwa pia nje ya mtandao wa intaneti kupitia apu ya simu ya rununu na kupitia ujumbe mfupi na mbinu nyingine. 
•    Washiriki pia waliulizwa maoni yao kupitia simu au kwa kupiga kura ambapo washiriki 50,000 katika nchi 50 walitoa maoni yao kupitia kupigia kura.
 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter