Uturuki chunguzeni ukiukwaji wa haki za binadamu Syria:OHCHR 

18 Septemba 2020

Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ameitaka serikali ya Uturuki kuanzisha uchunguzi mara moja ambao ni huru dhidi ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na ukatili uliotekelezwa katika baadhi ya sehemu za Kaskazini, Kaskazini Magharibi na Kaskazini Mashariki mwa Syria maeneo ambayo yako chini ya udhibiti wa vikosi vya Uturuki na makundi yenye silaha yaliyo na uhusiano na vikosi hivyo. 

Kamishina  Michelle Bachelet ameonya kwamba hali ya haki za binadamu katika maeneo kama Afrin, Ras al-Ain na Tel Abyad ni mbaya sana ikighubikwa na machafuko na vitendo vya kihalifu. 

Kwa mujibu wa ofisi ya haki za binadamu, “mwenendo wa kutia hofu wa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu umeorodheshwa katika maeneo hayo katika miezi ya hivi karibuni , vitendo kama ongezeko la mauaji, utekaji na usafirishaji kinyemela wa binadamu pamoja na upokonyaji wa ardhi na mali.” 

Waathirika wakubwa wa madhila haya ni pamoja na wale wanaochukuliwa kuwa ni wa upande wa upinzani, au wanaopinga makundi yenye silaha yaliyo na muingiliano na Uturuki ama walio matajiri wa kuweza kulipa kikombozi. 

“Watu wanaoishi katika maeneo haya ambao haki zao zimekiukwa wana haki ya kulindwa na kufidiwa. Kwa mantiki hiyo natoa wito kwa Uturuki kuanzisha mara moja uchunguzi wa kina, usioegemea upande wowote, wa wazi na huru dhidi ya matukio tuliyoathibitisha, kubaini hatima ya wanaoshikiliwa na waliotekwa na makundi yenye silaha yanayohusiana na Uturuki na kuwawajibisha waliohusika kwa ukiukwaji ambao wakati mwingine unachukuliwa kama ni uhalifu chini ya sheria za kimataifa ikiwemo uhalifu wa vita.” Amesema Bi. Bachelet. 

Ameongeza kuwa hili ni muhimu sana ikizingatiwa kwamba “tumepokea ripoti za kusikitisha kwamba baadhi ya mahabusu na watu waliotekwa wanadaiwa kuhamishwa na kupelekwa Uturuki baada ya kuwekwa rumande na makundi yenye silaha yaliyo na uhusiano na Uturuki.” 

Vifo na hatima ya raia 

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR tangu Januari mwaka huu imethibitisha takribani mauaji ya raia 116 katika maeneo hayo na wengine 463 waliojeruhiwa na vilipuzi na mabomu mengine ya kivita. Waliouawa ni pamoja na wanawake 15, wavulana 20 na wasichana wawili. 

Wafanyakazi wa ofisi hiyo pia wameorodhesha matukio ya utekaji na raia kutoweshwa, ikiwemo wanawake na watoto na hatima ya wengine bado haijulikani. 

Wakati huohuo ongezeko la mapigano miongoni mwa makundi yenye silaha kuhusu kushirikiana madaraka yamewaweka raia, maisha yao na miundombinu yao kwenye hatari kubwa. 

Makundi yenye silaha yaliyo na uhusiano na Uturuki pia yamepora na kushikilia nyumba, ardhi na mali zingine bila kuwepo na ulazima wa wanajeshi na wanaishi kwenye nyumba hizo na familia zao. 

 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter