Pamoja changamoto zilizopo, Umoja wa Mataifa hauna mbadala – Balozi Gastorn

18 Septemba 2020

Umoja wa Mataifa ukitimiza miaka 75 mwaka huu wa 2020 tangu kuanzishwa kwake, Tanzania, moja ya nchi 193 wanachama imesema chombo hicho hakina mbadala licha ya changamoto inazokikabili.
 

Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Kennedy Gastorn, amesema hayo jijini New York, Marekani wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, UN News Kiswahili kuelekea kuanza kwa mjadala mkuu wa ngazi ya juu wa mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, #UNGA75.

Profesa Gastorn amesema, “Umoja wa Mataifa uliundwa mwaka 1945 na nchi chache kama 55 hivi, na wakati huo Umoja huo uliundwa kutokana na uhalisia wa dunia uliokuwepo baada ya Vita Kuu ya pili ya Dunia,  nchi zilifikia hatua ambapo zilikubaliana kuwa haziwezi kuishi pamoja bila ya kuwa na chombo cha kuweza kuwaratibu na kuweza kuchukua dhamana ya kulinda amani na usalama duniani pamoja na mambo mengine.”

Akinukuu makatibu wakuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Balozi Gastorn amesema kuwa leo hii Umoja wa Mataifa unatimiza miaka 75, “nitakupa maneno mawili yaliyotolewa na makatibu wakuu waliopita, mmoja ni Dag Hammarskjöld, yeye alisema Umoja wa Mataifa hakuundwa kupeleka watu mbinguni lakini uliundwa kuwasaidia watu wasiende jehanamu. Mwingine ni Kofi Annan alisema Umoja wa Mataifa si chombo sahihi kilichokamiliki lakini hakina mbadala.”

Tanzania inaamini UN haina mbadala

Amesema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaamini kuwa Umoja wa Mataifa hauna mbadala lakini pia unaamini kuwa unahitaji maboresho endelevu ili umoja huo uweze kuwa na maana katika uhalisia wa sasa hivi, na uweze pia kutimiza malengo yake ya kuanzishwa kwake.

Mwakilishi huyo wa kudumu amesema, “sisi bado tunaamini katika Umoja wa Mataifa na tunaamini katika maboresho ya Umoja wa Mataifa, maboresho endelevu kutokana na uhalisi wa mabadiliko kuanzia mwaka 1945 na mpaka sasa. Mwaka 1945 zilikuwa nchi kama 55 kama nilivyosema leo kuna nchi wanachama 193.”

Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Kennedy Gastorn wakati wa mahojiano na Idhaa ya Umoja wa Mataifa.
UN News/Anold Kayanda
Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Kennedy Gastorn wakati wa mahojiano na Idhaa ya Umoja wa Mataifa.

Umoja wa Mataifa na Changamoto

Umoja wa Mataifa una changamoto, umeweza kuzuia migogoro mikubwa katika eneo la amani duniani, “kwa kweli hatujapata vita vya nyuklia ambavyo vilikuwa ni tishio kubwa sana wakati ule tunashukuru halijatokea.  Lakini kwa upande mwingine kuna migogoro midogo midogo mingi ambayo kwa kweli inapoteza maisha ya mamilioni ya watu kila siku. Hilo ni changamoto,”

Umoja wa Mataifa uliundwa ili kuleta maendeleo ya dunia, leo tunaona uchumi wa dunia hauko sawa. Nchi nyingi tajiri zinazidi kuwa tajiri na nchi nyingi maskini zinazidi kuwa maskini, hasa nchi zinazoendelea kutoka Afrika na kwingineko. 
Balozi Gastorn amesema, “Bado Umoja wa Mataifa unabidi ujitathmini illi kuweza kuleta uhalisia katika maisha ya watu kulingana na misingi yake ya mwaka 1945. Umoja wa Mataifa uliundwa mwaka 1945 kuleta usawa baina ya nchi, nchi kubwa, nchi ndogo, nchi yenye mabavu, nchi dhaifu baada ya kubaini kuwa vita havina mshindi, leo hii hatuoni uhalisia wa usawa baina ya nchi katika Umoja wa Mataifa.”

Taswira ya ukumbi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
UN Photo/Manuel Elías
Taswira ya ukumbi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Akifafanua kuhusu pengo la usawa ndani ya chombo hicho, Balozi Gastorn amesema “mwaka 1945 wakati Umoja wa Mataifa unaanzishwa kulikuwa na nchi 5 zenye kura turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Leo hii nchi hizo bado ziko 5 licha ya kwamba wanachama wameongezeka kutoka 55 hadi 193, mpaka leo Afrika haina kiti kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yenye turufu.”

Amesema pengo hilo la kura turufu kwenye Baraza la Usalama lipo ingawa kwamba, “wakati huo huo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, katika kazi zake kwa mwaka asilimia 75 ya kazi zote zinahusu Afrika. Afrika yenye watu asilimia 15 ya watu wote duniani, haina kiti kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Na ndio maana Jamhuri ya Muungano wa Afrika, mapendekezo yetu sisi ni yale yale ya kuungana na azimio la Afrika kwamba maboresho katika Baraza la Usalama ni muhimu na maombi yetu ni angalau walau tupate viti viwili kwenye eneo hilo.”

Ametamatisha akisema kuwa Umoja wa Mataifa umeweze kutekeleza mambo mengi, lakini yapo mengi yanayopaswa kufanyika lakini hauna mbadala.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter