Mikataba ya Ozoni ni mfano wa utashi wa kisiasa :Guterres 

16 Septemba 2020

Umoja wa Mataifa leo Jumatano umeadhimisha siku ya kimataifa ya kulinda tabaka la Ozoni kwa kutambua mafanikio ya kihistoria ya mikataba ya kimataifa katika kusaidia kukarabatio tabaka la Ozoni linalozunguka dunia. 

Katika ujumbe wake wa siku hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amepongeza mkataba wa Vienna wa 1985 kwa ajili ya kulinda tabaka la Ozoni, na kanuni zake zile za Montrieal Protocol na kanuni ya marekebisho ya Kigali protocol. 

“Mikataba ya kulinda tabaka la Ozoni ina mashiko na ni mfano wa kuigwa ambao unaonyesha kwamba palipo na utashi wa kisiasa hakuna linaloshindikana, hakuna ukomo wa kile tunachoweza kufikia kwa maslahi ya pamoja.” Amesema Guterres. 

Ni muhimu tukaelekeza juhudi zetu na uwekezaji katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kulinda maliasili na mifumo ya Maisha ambaye inatufanya tuishi-Katibu MKuu 

“Hebu na tuchagizwe na jinsi tulivyofanya kazi pamoja katika kulinda tabaka la Ozoni na kutumia utashi huohuo katika kuiponya dunia na kujenga mustakabali bora na sawa wa binadamu wote.” 

Katika zama hizi za janga la corona au COVID-19 na athari zake za kijamii na kiuchumi Katibu Mkuu ametaka kuwe na juhudi za kujenga jamiii imara na zenye mnepo. 

“Wakati tukiganga yajayo kwa dunia kujikwamua kutoka kwenye athari za kijamii na kiuchumi zilizosababishwa na COVID-19, ni lazima tujizatiti kujenga jamii imara na zenye mnepo zaidi” ameongeza Guterres. 

Amesisitiza kwamba ni muhimu kuweka juhudi pamoja na kuwekeza katika kukabiliana na mabnadiliko ya tabianchi na kulinda maliasili na mifumo ya Maisha ambayo inatuwezesha kuishi. 

Taarifa yake imesema mkataba wa Vienna kwa ajili ya kulinda tabaka la Ozoni ambao unaadhimisha miaka 35 mwaka huu ulikuwa ni hatua ya kwanza ya kuziba shimo katika tabala la ozoni la sayari dunia. 

Mwaka 1987 nchi zilipitisha mkataba wa montreal zikiahidi kubadili matumizi ya gesi zilizokuwa zikitumika vifaa vya kuhifahi baridi ambazo zilikuwa zinasababisha tobo kwenye tabaka hilo. 

Hadi kufikia sasa asilimia 99 ya gesi hizo zimebadilishwa na kusaidia uponyaji katika tabaka la Ozoni, lakini kazi ya mkataba wa montreal bado haijakamilika amekumbusha Bwana, Guterres. 

“Kupitia mkataba wa marekebisho wa Kigali, jumuiya ya kimataifa inasaka njia mbadala kwa mitambo ya baridi ambayo inachangia ongezeko la mabadiliko ya tabianchi. Endapo utatekelezwa kikamilifu mkataba wa Kigali utazuia ongezeko la joto dunia kwa nyuzi joto 0.4C. Nawapongeza wanachama 100 wa mkataba huo ambao wanaongoza kwa kuwa mfano” 

Ozoni ni nini? 

Ozoni ni aina ya mfumo wa Oksijeni inayojulikana kama O3. Hewa ya oksijeni tunayovuta duniani ni muhimu sana kwa maisha na inajulikana kama O2. 

Asilimia kubwa ya Ozoni inapatikana juu kabisa hewani kati ya kilometa 10-40 au maili kati ya 6-25 juu ya uso wa dunia. 

Eneo hilo linaitwa hewani na lina asilimia 90 ya ozone yote iliyoko hewani. 

Ingawa ni sehemu ndogo sana ya hewani lakini Ozoni ni muhimu kwa maisha ya dunia kwani inailinda dunia dhidi ya miozi ya jua ya ultraviolet UV-B. 

Siku ya kimataifa 

Mwaka 1994 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha tarehe 16 Septemba kuwa siku ya kimataifa ya kulinda tabaka la Ozoni ikiwa ni siku ya maadhimisho ya mwaka 1987 ya kutiwa sanini mkataba wa Montreal kuhusu kupinga vitu vinavyoathiri tabaka la Ozoni . 

Mwaka 2020 kauli mbiu ya siku hiyo ya kimataifa ni “Ozini kwa ajili ya maisha” ikiwa ni kumbusho kwamba Ozoni sio tu ni muhimu kwa ajili ya maisha duniani , bali pia ni lazima tuendelee kulinda tabala la Ozoni kwa ajili ya vizazi vijavyo. 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud