COVID-19 ni zaidi ya janga la kiafya, ni zahma ya kibinadamu:UN 

16 Septemba 2020

Akizindua ripoti hiyo kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa kwa njia ya mtandao Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema “hakuna nchi ambayo imenusurika, hakuna kundi la watu ambalo halijaguswa na gonjwa hilo na hakuna mtu aliye na kinga dhidi ya athari za janga hilo.” 

Ameongeza kuwa COVID-19 imepindua uchumi wa dunia na kughubika kivuli kwenye mustakabali wake, kwani kwa mujibu wa makadirio uchumi wa dunia utasinyaa kwa takriban asilimia 5 mwaka huu 2020 na watu wapatao milioni 100 wanaweza kusukumwa tena kwenye umasikini uliokithiri. 

Ripoti hiyo imesema mafanikio yaliyopatikana kwenye usawa wa kijinsia kwa miongo kadhaa sasa yako hatarini kugeuzwa huku maendeleo ya binadamu yakitarajiwa kushuka kwa mara ya kwanza tangu yalipoanza kupimwa mwaka 1990. 

Kwa upande wa Umoja wa Mataifa Katibu Mkuu Guterres amesema unatilia mkazo mambo matatu ambayo ni “mosi hatua za kiafya  ili kuokoa maisha, pili kupitisha sera za kulinda uhai, maisha na jamii na tatu mchakato wa kujikwamu ambao hautomuacha yeyote nyuma na unaoelekea kwenye dunia iliyo na usawa, mnepo na endfelevu baada ya COVID-19.” 

Ripoti pia imeongeza kuwa Umoja wa Mataifa ulijipanga mapema na kwa kina  na umeiongoza dunia katika kukabiliana na janga hilo ikiwa ni pamoja na kutoa msaada kwa walio hatarini zaidi. 

Kwa mujibu wa Guterres pamoja na hatua zote zilizofanyika “dunia bado iko katika awamu ngumu ya janga hilo na ili kuikabili inahitajika uongozi endelevu, ufadhili wa hali ya juu na mshikamano mkubwa baina na miongoni mwa nchi. Dunia inahitaji chanjo, upimaji na matibabu ambayo ni kwa kila mtu kila mahali. Chanjo ya COVID-19 ni lazima iwe kwa manufaa ya umma wote.” 

Amesisitiza kuwa pamoja na COVID-19 kuna janga lingine la kimataifa ambalo haliwezi kufumbiwa macho, ambalo ni mabadiliko ya tabianchi ambayo ripoti inasema linakwenda sanjari na COVID-19 na hatua kubwa na imara zinahitajika sasa kuliko wakati mwingine wowote ili kulinda na kuokoa maisha ya mamilioni ya watu dhidi ya janga hilo.

Ametooa wito kwamba “ni lazima kubadili na kuimarisha miundombinu ya ushirikiano wa kimataifa ili tuwe katika maandalizi bora zaidi janga lingine kama hili litakapozuka. Ni muhimu kuimartisha maandalizi dhidi ya majanga, udhibiti wake na hatua za kukabiliana nayo. Endapo dunia haitochukua hatua dhidi ya maambukizi yatokanayo na wanyama basi majanga kama COVID-19 yatakuwa kitu cha kawaida.” 

 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter