Watu 650,000 wameathirika na mafuriko yanayoendelea nchini Sudan kufuatia mvua kubwa zilizoanza kunyesha tangu mwezi Julai na juma hili pekee watu wengine 110,000 wametawanywa na sasa wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu limesema shirika la Umoja wa Mataifa la msaada wa kibinadamu na masuala ya dharura OCHA.
Kwa mujibu wa taarifa ya shirika hilo iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi mvua kubwa zimeongezeka katika nchi nzima ya Sudan wiki iliyopita na kusababisha mafuriko makubwa, watu kutawanywa na vifo, na hivyo kuifanya serikali ya nchi hiyo kutangaza hali ya dharura kwa nchi nzima kwa kipindi cha miezi mitatu.
OCHA inasema maelfu kwa maelfu ya watu waliotawanywa wengi sasa wanapata hifadhi mashuleni na hivyo kuzusha changamoto nyingine kwa serikali na walimu wakati huu shule zikikaribia kufunguliwa.
Serikali na washirika wengine wa misaada wamekuwa wakiwasaidia watu 200,000 katika maeneo yaliyoathirika zaidi lakini mafuriko hayo yamepindukia matarajio na sasa washirika hao wanaishiwa misaada ya kuencdelea kuwasaidia waathirika.
Ukurasa kuhusu virusivyacorona & taarifa mpya
Wasomaji wanaweza kupata taarifa na muongozo kuhusu mlipuko wa virusi vya corona (2019-nCoV) kutoka Umoja wa Mataifa, Shirika la afya duniani na mashirika mengine ya UN hapa. Kwa habari mpya kila siku kutoka UN News, bofya hapa.
Kwa mujibu wa OCHA utabiri unaonyesha kwamba hali itaendelea kuwa mbaya zaidi hasa kwa kuwa mvua kubwa zinaendelea kutarajiwa nchini Ethiopia na sehemu mbalimbali za Sudan ambazo zina uwezekano mkubwa wa kusababisha maji kufurika na kupandisha kina ncha mto Blue Nile hali ambayo itasababisha mafuriko makubwa na uharibifu.
Takwimu zinaonyesha kwamba watu wengi zaidi wameathirika na mafuriko mwaka huu kuliko miaka mingine saba iliyopita.