Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi 10 wauawa na 19 wajeruhiwa Uganda, UNHCR yataka uchunguzi 

Wakimbizi wa Sudan Kusini waliopo nchini Uganda
WFP/Henry Bongyereirwe
Wakimbizi wa Sudan Kusini waliopo nchini Uganda

Wakimbizi 10 wauawa na 19 wajeruhiwa Uganda, UNHCR yataka uchunguzi 

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema limeshtushwa na kutiwa hofu na kitendo vya machafuko yaliyosababisha vifo vya wakimbizi 10 na kujerughi wengine 19 ikiwemo mtu mmoja kutoka katika jamii zinazohifadhi wakimbizi hao kwenye eneo la Madi wilaya ya Okollo Kaskazini mwa Uganda. 

Katika taarifa yake iliyotolewa leo UNHCR imesema kwa mujibu wa taarifa ilizozipokea hadi sasa, Ijumaa ya septemba 11 mwaka huu kwenye majira ya saa 11 jioni saa za Afrika Mashariki mzozo ulizuka baina ya wenyeji na wakimbizi karibu na kituo cha maji kinachotumika na pande mbili hizo na kisha ukageuka machafuko na mashambulizi dhidi ya wakimbizi kwenye Kijiji cha Tika kilichoko makazi ya wakimbizi ya Rhino ambako wakimbizi kutoka Sudan Kusini wanaishi. 

Mbali ya machafuko hayo kusababisha idadi kubwa ya vifo na mjeruhi nyumba 15 za wakimbizi zimeteketezwa kabisa kwa moto na zingine 26 zimethibitishwa kuporwa na kuharibiwa. 

UNHCR imeongeza kuwa inatiwa hofu kubwa kuhusu usalama wa wakimbizi wengine 10 ambao bado hawajulikani waliko na imetoa wito kwa mamlaka kuwasaka mara moja. 

Tunatoa pole kwa familia za waliopoteza maisha na kuwatakia ahuweni ya haraka majeruhi. Machafuko haya ya kupindukia yanayofanywa na jamii zinazohifadhi wakimbizi kwa sababu ya mzozo wa kijamii yanatoa ishara ya tishio kwa uwiano wa amani ya kuishi pamoja kwenye maeneo ya vijijini ambako wakimbizi wanaishi pamoja na wenyeji wa Kiganda.” Amesema Joel Boutroue mwakilishi wa UNHCR nchini Uganda.

Bwana Boutroue ameongeza kuwa, “katika mazingira yenye uhaba wa rasilimali matukio ya janga kama lililotokea Ijumaa iliyopita yanatia wasiwasi mkubwa kwani wote wenyeji na wakimbizi wanakabiliwa na ugumu wa maisha kwa kupungua kwa fursa za upatikanaji wa hudumu za msingi na uwezo wa kujikimu kimaisha.” 

UNHCR imetoa wito wa kurejesha utulivu wakati huu ikishirikiana na mamlaka kuhakikisha kwamba hatua zaidi za usalama zimeimarishwa na tukio hilo la mauaji linachunguzwa kwa kina ili kusaidia kuweka bayana mazingira yaliyosababisha ikiwemo jukumu la malaka za eneo hilo. 

UNHCR imepeleka mara moja timu kwenye eneo hilo kusaidia wakimbizi ambao wamepata kiwewe kutokana na shambulio hilo na kushirikiana na serikali na washirika wengine kusaidia kukidhi mahitaji ya walioathirika huku wakichagiza juhudi za maridhiano.