Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kwa mara ya kwanza pande kinzani Afghanistan zakutana uso kwa uso

Maadhimisho ya miaka 100 ya Uhuru wa afghanistan yalisherehekewa kwenye mji wa Kandahar mwezi agosti 2019 kwa mamia ya watu kuandamana na bendera za taifa lao mitaani
UNAMA / Mujeeb Rahman
Maadhimisho ya miaka 100 ya Uhuru wa afghanistan yalisherehekewa kwenye mji wa Kandahar mwezi agosti 2019 kwa mamia ya watu kuandamana na bendera za taifa lao mitaani

Kwa mara ya kwanza pande kinzani Afghanistan zakutana uso kwa uso

Amani na Usalama

Mazungumzo ya kwanza kabisa ya uso kwa uso kati ya wawakilishi wa serikali ya Afghanistan na wale wa kikundi cha Taliban ambayo yameanza hii leo Jumamosi ni fursa kuwa ya kuwezesha kufikia matarajio makubwa ya amani nchini humo.
 

Ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres aliyotoa leo kwa njia ya video mwanzoni mwa mazungumzo hayo huko Doha nchini Qatar.

Guterres amesema wito wa mara kwa mara wa hatua za wananchi wa Afghanistan wenyewe kumaliza ghasia na kuweka fursa ya kusongesha nchi yao baada ya kuacha mapigano ni msingi wa uzinduzi wa mkutano wa leo.
Katibu Mkuu ameshukuru serikali ya Qatar kwa kuwe mwenyeji wa mazungumzo hayo.

Mchakato jumuishi
 

UNnewsVideo
Kwenu wana Afghanistan

“Waafghanistan wenyewe wanapaswa kuchambua na kupanga mchakato wa mashauriano yao. Mchakato wa amani jumuishi ambamo wanawake, vijana na manusura wa mzozo wa Afghatanistan wanawakilishwa ipasavyo unatoa matumaini bora zaidi ya suluhu endelevu,” amesema Katibu Mkuu.

Taifa hilo la barani Asia kwa miongo minne limegubikwa na mapigano yaliyosababisha vifo vya maelfu ya watu na hadi sasa hakukuwahi kuwepo kwa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya kikundi hicho cha Taliban kilichokuwa kinadhibiti nchi hiyo kabla ya kupinduliwa na Marekani na washirika wake mwaka 2001 na hatimaye kufanyika kwa uchaguzi wa kidemokrasia ulioweka serikali madarakani.

Mkuu huu wa leo umefanyika kufuatia makubaliano ya usalama kati ya Marekani na wawakilishi wa Taliban mwezi Februari mwaka huu ambao ulifungua njia. Mwendelezo wa ghasia na kusuasua kwa utekelezaji wa masharti kama vile kubadilishana wafungwa kuliendelea kutishia kufanyika kwa mazungumzo.

Akisisitiza umuhimu wa kujumuisha wanawake, Katibu Mkuu Guterres amesema pande zote lazima zihakikishe kuwa wanawake wanashiriki katika dhima mbalimbali kwenye mchakato wa amani kwa kuakisi uzoefu na utaalamu wao kwenye maisha yao ya kila siku na utofauti wao kwenye jamii hiyo.

Ulinzi wa raia

Amegusia pia makubaliano mawili ya karibuni ya kusitisha mapigano akisema yalitoa ishara ya kutia moyo lakini wakati huu ambapo mazungumzo yanaendelea, “nasihi juhudi ziongezwe maradufu katika kulinda raia na kupunguza mizozano ili kuokoa maisha na kuweka mazingira bora zaidi ya mazungumzo.”

Guterres amesema ni matumaini yake kuwa maendeleo kuelekea amani yatakuwepo na kuweza kupatikana kwa amani ya kuwezesha kurejea nyumbani kwa mamilioni ya wananchi wa Afghanistan walio wakimbizi ndani na nje ya nchi yao.

Amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa inashikamana na taifa hilo na itafanya kila liwezekanalo kusaidia mchakato huo wa amani unaoongozwa na wananchi wenyewe wa Afghanistan.