Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya usalama eneo la Irumu, DRC yamtia hofu Guterres

Kamanda wa kikosi cha Tanzania huko DRC, Luteni Kanali John Ndunguru (katikati) katika mazungumzo na afisa wa jeshi la DRC, FARDC huko Beni, DRC.
TANZBATT 7/Ibrahim Mayambua
Kamanda wa kikosi cha Tanzania huko DRC, Luteni Kanali John Ndunguru (katikati) katika mazungumzo na afisa wa jeshi la DRC, FARDC huko Beni, DRC.

Hali ya usalama eneo la Irumu, DRC yamtia hofu Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameelezea wasiwasi wake juu ya mwendelezo wa ghasia katika eneo la Irumu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
 

Eneo husika zaidi ni kwenye mipaka ya jimbo la Kivu Kaskazini na Ituri.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric, kupitia taarifa aliyoitoa Ijumaa usiku jijini New York, Marekani amemnukuu Katibu Mkuu Guterres akisema “mashambulio ya hivi karibuni kwa mara nyingine tena yamesababisha vifo vya raia. Eneo hilo limeendelea kukumbwa na mapigano ya kikabila lakini pia vitisho kutoka waasi wa kikundi cha Allied Democratic Forces, ADF.”

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kusaidia mamlaka za DRC katika kuwafikisha mbele ya sheria wahusika wa vitendo hivyo vya mashambulizi dhidi ya raia, vikosi vya ulinzi pamoja na walinda amani.

“Amesisitiza azma ya Umoja wa Mataifa ya kusaidia jitihada za serikali ya DRC katika kujenga amani na utulivu mashariki mwa nchi hiyo,” imesema taarifa hiyo.

Walinda amani wanawake kutoka Tanzania katika mazungumzo na mwanamke mkazi wa Beni, nchini DRC.
TANZBATT 7/Ibrahim Mayambua
Walinda amani wanawake kutoka Tanzania katika mazungumzo na mwanamke mkazi wa Beni, nchini DRC.

Vitendo vya ukatili

Kwa mujibu wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, ADF wamekuwa wakiimarisha mashambulizi yao dhidi ya raia kwenye eneo hilo la mashariki mwa DRC katika kipindi cha miezi 18 iliyopita.

Maelfu ya watu wameuawa wengine mamia kadhaa wamejeruhiwa na kwamba vitendo hivyo vinaweza kuwa uhalifu dhidi ya binadamu.

Kwa zaidi ya miongo mitatu, ADF wamekuwa wamekifanya mashambulizi kwenye mji wa Beni jimboni Kivu Kaskazini lakini kufuatia kampeni za kijesih dhidi ya kikundi hicho tangu mwezi Oktoba mwaka 2019, wapiganaji wake wamesambaa katika vikundi vidogo vidogo na kukimbilia eneo la Irumu mpakani na jimbo la Ituri ambako sasa ndio wameimarisha mashambulizi yao.

Waasi hao wamekuwa wakishambulia vijiji wakitumia silaha nzito kama vile AK47 na makombora, visu na mapanga ambako mara nyingi huteketeza vijiji, huharibu vituo vya afya, shule na kuteka na kutumikisha wanaume, wanawake na watoto kwenye vikundi vyao.