Mafuriko yahamisha watu na kutwamisha miundombinu Sudan

11 Septemba 2020

Nchini Sudan mvua kubwa zimesababisha mafuriko na kuharibu miundombinu huku watu zaidi ya 557,000 wakiwa hawana makazi na nyumba zaidi ya 111,000 zikisombwa kwa maji.

Umoja wa Mataifa kupitia mashirika na taasisi zake unasema kwamba watu hao ni katika majimbo 17 kati ya 18 ya Sudan na majimbo yaliyoathirika zaidi ni Khartoum, Darfur Kaskazini na Sennar, yakijumuish asilimia 43 ya wananchi wote walioathirika.

Taarifa ya kamisheni ya usaidizi wa kibinadamu, HAC, inanyumbua kiwango cha uharibifu ambao ni pamoja na kuharibiwa kwa ekari 1,700 za ardhi ya kilimo, majengo 179 ya shule, vituo vya afya na ofisi za serikali huku maduka na bohari 359 zikisombwa kwa maji na mifugo 5,500 imekufa.

Halikadhalika madaraja yamesombwa kwa maji, barabara kuu nazo zimetwama.

HAC inaonya kuwa uharibifu zaidi unatarajiwa kutokea kwa kuwa mafuriko zaidi yanaweza kutokea katika siku chache zijazo kwenye mto Nile na majimbo ya kaskazini nchini Sudan.

Mahitaji ya dharura

Kinachohitajika sasa ni malazi, vyakula na huduma za kujisafi na maji safi ili kuepusha magonjwa ya kuhara.

Tayari ndege imewasili kutoka Falme za kiarabu ikiwa na vifaa vya misaada.

HAC iko chini ya serikali ya Sudan n aina wajibu wote wa kushughulikia jamii wakati huu wa janga la mafuriko huku jamii ya kimataifa ikiwa na dhima ya msingi ya usaidizi na tathmini ya mahitaji ya dharura.

Mapema akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini Geneva, Uswisi, msemaji wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, Fadela Chaib amesema kuwa kufuatia mafuriko nchini Sudan, wanapeleka msaada wa vifaa vya upasuaji na dawa za kutibu kipindupindu na magonjwa mengine kwa jamii zilizoathirika.

Bi. Chaib amesema maafisa 10 wa mazingira wamepelekwa kwenye maeneo mbalimbali nchini Sudan kusaidia mamlaka za serikali kwenye huduma safi za maji na za kujisafi na kuepusha mazalia ya vijidudu.

Hivi sasa WHO inasaidia magari 10 yenye kliniki za kuhamahama kwenye mto wa Blue Nile, Kassala na Darfur Kati na wana mpango wa kupeleka huduma kama hiyo siku chache zijazo kwenye jimbo la Khartoum.

Kwa kushirikiana na wadau na serikali ya Sudan, WHO imebaini mahitaji ya kiafya na kushughulikia miito ya dharura 128 ikiwemo ya kipindupindu, surua, COVID-19 na mengineyo.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter