Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

TANZBATT-7 yatumia sanaa kuimarisha amani DRC

Kikundi cha utamaduni cha walinda amani kutoka Tanzania kikifanya onesho kwenye mji wa Beni jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
TANZBATT 7/Ibrahim Mayambua
Kikundi cha utamaduni cha walinda amani kutoka Tanzania kikifanya onesho kwenye mji wa Beni jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

TANZBATT-7 yatumia sanaa kuimarisha amani DRC

Amani na Usalama

Sanaa katika operesheni za ulinzi wa amani zinazofanywa na Umoja wa Mataifa kwenye mataifa mbalimbali ikiwemo Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC imedhihirika  kuwa mbinu muhimu ya kuleta utangamano miongoni mwa wanajamii wa taifa hilo hususan jimboni Kivu Kaskazini kwa kuwa na ujumbe maridhawa wa amani kwa rai na kusahau magumu wanayopitia  kufuatia machafuko yaliyodumu kwa miongo kadhaa.
 

Mbinu hiyo ya Sanaa katika ulinzi wa amani inatumiwa na walinda amani kutoka Tanzania wa kikundi cha 7 cha walinda amnai kutoka Tanzania, TANZBATT-7 wanaohudumu kwenye kikosi cha kujibu mashambulizi, FIB, cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO.

Miongoni mwa ujumbe mahususi  unaobebwa na sanaa hii ya ngoma za asili kutoka katika kikundi cha sanaa  cha Upendo kutoka Tanzania ni kudumisha amani na upendo  miongoni mwao, amani ambayo imetetereka kwa muda mrefu hivi sasa.
Sajini Hamisi Yoba, mkufunzi wa kikundi cha sanaa, ni miongoni mwa walinda amani na kiongozi wa kikundi cha Upendo , ambaye anathibitisha  mapokeo ya sanaa kwa hapa DRC na kusema kuwa sana imeonesha kujenga ukaribu mkubwa kwa jamii na walinda amani hasa kwa ujumbe unaowasilishwa.

Kikundi cha utamaduni cha Upendo cha walinda amani wa Tanzania nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, ambacho hutumia ngoma kuimarisha amani.
TANZBATT 7/Ibrahim Mayambua
Kikundi cha utamaduni cha Upendo cha walinda amani wa Tanzania nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, ambacho hutumia ngoma kuimarisha amani.

“Sisi tunapokwenda kufanya maonesho yetu, hawataki tumalize maonesho, wanataka tukeshe tukiwapatia burudani. Mapokeo ya sanaa yamekuwa makubwa kuliko ambavyo ninaweza kuelezea,” amesema Sajini Yoba.

Anaeleza kuwa kupitia sana imewezesha walinda amani kuifikia jamii kubwa kiurahisi zaidi ikilinganishwa na hapo awali ambapo ilikuwa ni vigumu kutokana na machafuko yaliyodumu kwa muda mrefu na hivyo anatoa wito kwa wana DRC akisema, “kwa wananchi wa DRC, amani ni kitu pekee na ndio kitu ambacho kitawajumuisha pamoja, natoa wito muilinde amani.”

Sanaa ya ngoma za asili imejizolea umaarufu mkubwa nchini DRC, ambapo mpaka sasa imekuwa ikifanya vizuri katika matamasha ya kuhamasisha amani na maadhimisho ya siku za Kimataifa  kama vile siku ya wanawake duniani na  ya Umoja wa mataifa.

Assumpta Massoi/UNNewsKiswahili
Tukianza hawataki tumalize, wanataka tusilale- TANZBATT-7