Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ufadhili, umoja na kuaminiana ni mambo ya lazima kwa ajili ya chanjo ya COVID-19: UN 

Mtaalamu wa maabara akifanya kazi katika kituo cha afya na sayansi mjini Bngkok, Thailand.
WHO/P. Phutpheng
Mtaalamu wa maabara akifanya kazi katika kituo cha afya na sayansi mjini Bngkok, Thailand.

Ufadhili, umoja na kuaminiana ni mambo ya lazima kwa ajili ya chanjo ya COVID-19: UN 

Afya

Viongozi mbalimbali wa Dunia leo Alhamisi wametetea chombo cha kusongesha fursa za nyenzo za kupambana na janga la corona au COVID-19 (ACT Accelerator) wakati huu janga hilo likiendelea kutatiza kote duniani.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO Dkt. Tedros Adhanon Ghebreyesus ndiye aliyeileta pamoja jumuiya ya kimataifa katika suala hii akitarajia uongozi wao wa hali ya juu wa kisiasa kuja na hatua za pamoja kushughulikia virusi vya corona kupitia ACT Accelerator. 

Akiungwa mkono na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa , Rais wa tume ya Muungano wa Ulaya, waziri mkuu wa Norway na marais wa Afrika Kusini na Rwanda, mkurugenzi mkuu wa WHO amedhamiria kusaka suluhu ya kimataifa dhidi ya COVID-19 wakati huu ambapo kuna jitihada na mikakati mbalimbali inafanyika. 

ACT Accelerator ambayo ilizinduliwa mwishoni mwa mwezi Aprili “ni ushirikiano wa kimataifa wenye lengo la kuchapuza maendeleo na uzalishaji wa bidhaa za upimaji, matibabu na chanjo dhidi ya COVID-19 na kuhakikisha fursa sawa kwa wote.” 

Zaidi ya miezi minne tangu kuzinduliwa chombo hicho Dkt. Tedros amepongeza kasi ya utengenezaji wa bidhaa hizo akisema, “hivi sasa tunaandaa muafaka kuhusu usambazaji wa kimataifa wa bidhaa hizo. Lakini ACT Accelerator haiwezi kutimiza malengo yake bila kuongeza ufadhili.” 

Leo hii mkakati huu ambao unayaleta pamoja mashirika mbalimbali ya kimataifa yanayojikita na masuala ya afya na ufadhili, umepokea dola bilioni 2.7. Kiwango ambacho kimewezesha kuanza kwa mchakato awamu ya kwanza lakini kinawasilisha chini ya asilimia 10 ya ya mahitaji yote. 

Katibu Mkuu Antonio Guterres amesisitiza kwamba “tunahitaji dola bilioni 35 kusongesha mchakato huu mbele na kuleta ufanisi. Kwani muda unatutupa mkono endapo hazitopatikana dola bilioni 15 katika miezi mitatu ijayo , dunia itakuwa hatarini kupoteza fursa ya kusongesha mbele utafiti dhidi ya virusi hivyo. Wahisani ni lazima watumie fedha ambazo tayari zimeshaidhinishwa ili kushambulia janga la COVID-19 katika nyanja zote.” 

Hakikisho la fursa sawa za chanjo 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekumbusha kwamba tatizo la la ufadhili wa nyenzo za kupambana na COVID-19 liliongezwa na suala la uratibu. Nchi kadhaa ziliamua kukabiliana na virusi vya corona katika njia mbalimbali  kwa lengo la kulinda maslahi ya mataifa yao, bila kujali kwamba janga hilo ni adui wa pamoja wa kimataifa. 

Bwana Guterres amesisitiza kwamba “chanjo yoyote itakayopatikana dhidi ya virusi hivyo ni lazima iwe ya gharama nafuu kwa maslahi ya umma wa Dunia na ipatikane kwa watu wote kwa sababu janga la COVID-19 halibagui, halichagui na haliheshimu mipaka.” 

Mwenyekiti mwenza wa baraza la uwezeshaji la ACT Accelerator , Rais wa Afrika Kusini amekuwa akipigia upatu nchi za kusini ambazo mara nyingi zinakosa rasilimali za kupambana na virusi vya corona. 

Bwana Cyril Ramaphosa ambaye nchi yake ndio Rais wa Muungano wa Afrika mwaka huu  amesema “hatuwezi kufikia huduma za afya kwa wote wakati chanjo ya COVID-19 inapatikana tu kwa nchi zenye rasilimali kwa minajili ya utafiti, utengenezaji, usambazaji na huduma.” 

Mwenyekiti mwenza mwingine wa baraza hilo ambaye ni waziri mkuu wa Norway Erna Solberg amesisitiza kwamba “fursa sawa za chanjo hizo ni suala la haki za binadamu  na usalama wa afya ya kimataifa. Asante kwa ACT Accelerator kwani serikali, mashirika, viwanda na asas iza kijamii ni lazima zishikamane sasa kuliko wakati mwingine wowote kuchapuza mchakato wa kutengeneza chanjo, upimaji na matibabu.” 

Kwa upande wake Rais wa Rwanda Paul Kagame ambaye anaongoza ushirika mpya kwa ajili ya afrika NEPAD ameipongeza pia ACT acceerator ambayo "kwa kupunguza hatari imewezesha hakikisho la usawa katika usambazaji na upatikanaji.” 

Naye Rais wa tume ya muungano wa Ulaya Ursula von de Leyen ameahidi ahadi ya Muungano wa Ulaya ya “kutumia nguvu zake zote kusidia kuhakikisha umoja wa jumuiya ya kimataifa dhidi ya virusi hivyo. Wakati Rais wa Norway na Afrika Kusini wakiwasilisha Kaskazini na Kusini, na kwa utaalam wa WHO na washirika wetu wa kimataifa , hakuna nchi au ukanda ambao utaachwa nyuma katika vita hivi.” Amesisitiza rais huyo. 

Mbali ya ufadhili na juhudi za uratibu, Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza umuhimu wa kujenga imani katika chanjo. 

“Ili chanjo iweze kufanya kazi asilimia kubwa ya wanaume, wanawake na watoto kote duniani lazima wawe tayari kuitumia. Kwani kutokuwa na imani, kusita, na dhana potofu kuhusu chanjo hiyo kwa ujumla vinaongezeka kote duniani.  

Kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu ametangaza kwamba Umoja wa Mataifa na WHO wanashirikiana kwa karibu na vyombo vikubwa kupambana na taarifa potofu ambazo zinazagaa kwenye mitandao ya kijamii.