Sasa wachambua taka Afrika kusini wafanya kazi kwa kujiamini, kulikoni?

10 Septemba 2020

Nchini Afrika Kusini, shirika la Umoja wa Mataifa la maendeleo ya viwanda, UNIDO na serikali ya Japani limefanikisha usaidizi wa mavazi ya kujikinga mwili kwa waokota na wachambuzi taka ngumu nchini humo ili kuwaepusha na maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 . 

Hatua hiyo ya serikali ya Japan imekuja baada ya taifa hilo la Asia kutaka kusaidia nchi za Afrika kuepukana na taka ngumu kuchafua baharí kwa kuondokana na matumizi ya plastiki za kawaida na badala yake kutumia bidhaa ambazo ni endelevu. 

Katika mchakato wa kuchambu ni bidhaa gani zinaweza kuwa mbadala ndipo mradi ukaangalia pia wazoa taka ambao ni muhimu sana katika mnyororo mzima kuanzia kuokota taka hadi kuziwasilisha pahala salama pa kuzirejeleza. 

UNIDO iliona ni vyema mradi ukawagusa waokota taka kwa kuwa iwapo bidhaa zitabadilishwa pengine hawatakuwa na taka za kurejeleza au katika kuchambua wafahamu jinsi ya kuzitenganisha. 

Simon Mbatha ni mwenyekiti wa chama cha wazoa taka Afrika Kusini, SAWPA na anasema, “kwa manispaa nyingi, COVID-19 ilipokuwa kiwango cha 4, kwa wazoa taka kuweza kurudi kwenye dampo la kiwango kikubwa kama la kwetu, walitakiwa kuwa na mavazi ya kujikinga, PPE, na wengi wao hawakuweza kurudi kazini. Wazoa hata hawana ajira ya kuweza kupatiwa PPE.” 

Dkt. Melanie Samson kutoka Chuo Kikuu cha Witz nchini Afrika Kusini anasema kuwa kwa miaka kadhaa wazoa taka wamekuwa wakilalama kuwa wanafanya kazi hii bila vifaa vya kujikinga, na kwa kuzingatia kuwa wanachambua majalala ili kutenganisha taka ilikuwa ni lazima katika zama hizi ambapo virusi vya Corona vinaweza kuwepo pahala kwa muda mrefu. 

Kwa kupatiwa vifaa hivyo wanaweza kuendelea kufanya kazi na wakati huo huo kuendelea kutunza familia zao. 

Baada ya PPE kupatiwa maeneo manne ya kusomba na kuchambua taka, Bwana Mbatha anasema,  "hebu nishukuru UNIDO kwa msaada wake hadi sasa, hii imekuwa changamoto kubwa sana kwa wazoa taka, PPE imekuwa ni tatizo. Hata sasa bado si salama, kila siku tunakuwa na vikao ili kila mtu aelewe  kwa sababau virusi vinaweza kuwepo katika taka tunazochambua.” 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter