Mtandao wa maabara mahsusi za kunyumbua virusi vya Corona yazinduliwa Afrika

10 Septemba 2020

Wakati nchi za Afrika zikiendelea kupanua huduma za upimaji wa virusi vinavyosababisha Corona au COVID-19, shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO na kituo cha Afrika cha udhibiti na kinga ya magonjwa, Africa CDC, wamezindua mtandao wa maabara ili kuimarisha hatua za kuchambua na kufuatilia mnyumbuliko wa virusi vya Corona aina ya 2 kinachosababisha shida kwenye mfumo wa hewa, SARS-CoV-2.
 

Taarifa ya WHO kanda ya Afrika iliyotolewa katika miji ya Addis Ababa, Ethiopia na Brazaville, Congo imesema kuwa, virusi aina hiyo ndio vinasababisha , ambacho kinasababisha ugonjwa wa COVID-19 barani Afrika.
Maabara 12 mahsusi kwa ajili ya mpango huo zimo kwenye mtandao huo na zitatoa uchambuzi wa SARS-CoV-2 kuanzia uchambzi wa taarifa za virusi hivyo, na msaada mwingine wa kiufundi kwa nchi ambako maabara hizo zimo au kwa nchi jirani na maeneo mengine ya kikanda kwenye bara hilo la Afrika.

Akizungumzia hatua hiyo, Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika, Dkt. Matshidiso Moeti amesema, “tunapoendelea kushughulikia janga la COVID-19 barani Afrika, kuwa na uwezo wa sio tu kufuatilia mabadiliko ya virusi hivi, bali pia kutathmini uwezo wake wa kujibadili ni muhimu katika kupata tiba sahihi.”

Mwanafunzi wa kike nchini Ghana akinawa mikono kwa sabuni kabla ya kurejea darasani ikiwa ni sehemu ya mpango wa serikali kuhakikisha elimu inaendelea huku wakidhibiti maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.
UNICEF/Geoffrey Buta
Mwanafunzi wa kike nchini Ghana akinawa mikono kwa sabuni kabla ya kurejea darasani ikiwa ni sehemu ya mpango wa serikali kuhakikisha elimu inaendelea huku wakidhibiti maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.

Amesema kwamba kupitia maabara hizo zilizojikita kwenye uchambuzi wa virusi hivyo, “tunaweza kutengeneza chanjo na tiba ambazo zitaendana na mazingira ya Afrika na hatimaye kuweza kudhibiti COVID-19.”
Hatua zinazoendelea hivi sasa za kuchambua virusi hivyo zimetoa taarifa muhimu za kutambua virusi aina ya SARS-CoV-2 vinavyoenea katika baadhi ya nchi.

Virusi vinavyosababisha COVID-19 Afrika ni kama vya Ulaya

Uchambuzi mathalani umeonyesha kuwa, aina ya SARS-CoV-2 iliyoenea barani Afrika ni B.1 ambayo chimbuko lake ni janga la COVID-19 barani Ulaya.
Barani Afrika aina 10 za virusi hivyo SARC-CoV-2 vimetambuliwa na zaidi ya minyumbuliko 800,000 imeshatambuliwa duniani kote.

Maabara hizi zitatusaidia kutengeneza chanjo na tiba iendanayo na mazingira ya Afrika - Dkt. Moeti

Kwa kuweka kwenye makundi virusi kutoka mataifa mbalimbali kwenye msururu mmoja kumedokeza uhusiano au uwezekano wa kuhamisha virusi kutoka nchi moja kwenye nyingine.

WHO inasema kuwa nchi kama vile Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Afrika Kusini zina tatizo la maambukizi ya ndani ya COVID-19 ambako pia kuna virusi kutoka nje nje kama vile kutoka Ghana, Morocco na Senegal.
Africa CDC na WHO kwa pamoja wanapatia nchi wanachama vifaa vya kusaidia kunyumbua virusi hivyo vinavyosababisha COVID-19 pamoja na vitendanishi sambamba na msaada wa kiufundi.

Hadi sasa jumla ya minyumbuo 2016 ya SARC-CoV-2 imebainika katika mataifa 18 ya Afrika ambayo ni  Algeria, Benin, Cameroon, DRC, Misri, Gambia, Ghana, Kenya, Madagascar, Mali, Morocco, Nigeria, Senegal, Sierra Leone, Afrika Kusini, Tunisia, Uganda, na Zambia.

Kupitia mnyumbuliko huo, itakuwa rahisi kwa nchi husika kutambua jinsi ya kushughulikia COVID-19 na kudhibiti maambukizi ya ndani ya nchi zao.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter