Wana CAR wataka uchaguzi ufanyike kwa amani 

10 Septemba 2020

Kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR tarehe 27  mwezi Desemba mwaka huu, wapiga kura kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Bangui wametoa maoni yao wakati huu ambapo tayari kazi ya kuandikisha wapiga kura ilianza mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu. 

Wapiga kura hao wakihojiwa na Radio Guira FM ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini CAR, MINUSCA wamesema, “ni wakati wa kila mwana CAR kupima thamani ya kila mgombea ambaye anataka kuongoza mustakabali wao. Kwa hiyo tunapenda chaguzi hizo zifanyike kwa utulivu na amani.” 

Kwa mkazi mwingine wa Bangui suala muhimu ni uchaguzi uwe huru akisema, “ni kuwaachia wana Jamhuri ya Afrika ya Kati wapige kura kwa uhuru na tuzingatie matokeo ya chaguzi hizo na kati wasituchagulie mtu ili kipindi cha uchaguzi kiweze kupita salama.” 

Wagombea nao wakapatiwa wito na mkazi mwingine wa Bangui ambaye yeye anasema, “natoa wito kwa wote, wapiga kura, wagombea n apande zote, tukumbuke kuwa sote tu wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Sote tunakwenda kwenye uchaguzi na vita havitusongeshi popote. Tufanye chaguzi kwa amani na tuendelee kuishi kwa amani.” 

Katika miezi ya hivi karibuni, nyaraka na vifaa vya uchaguzi viliwasili nchini humo ikiwemo kompyuta ndogo za dijitali 4,400 kwa ajili ya kuandikisha wapiga kura, vibanda vya kupigia kura, paneli za sola na betri pamoja na vifaa vya kuhifadhi umeme na vifaa vyote hivyo vimesambazwa kote nchini CAR kwa usaidizi wa MINUSCA. 

Azimio la Baraza la Usalama la  Umoja wa Mataifa namba 2499 linapatia MINUSCA jukumu la kusaidia mamlaka za CAR katika maandalizi na kufanyika salama kwa uchaguzi huo ujao. 

Kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi, iwapo katika awamu ya kwanza ya uchaguzi war ais tarehe 27 mwezi huu hakutakuwa na mshindi anayepata zaidi ya asilimia 50 ya kura zitakazopigwa, basi awamu ya pili itafanyika tarehe 14 mwezi Februari mwaka 2021. 

Uchaguzi mkuu wa mwisho ulifanyika nchini humo mwaka 2015/2016. 

 

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter

Fuatilia Habari: Habari zilizopita za Mada Hii

Shehena nyingine ya vifaa vya uchaguzi yawasili CAR

Nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR,  shehena ya tatu ya vifaa vya uchaguzi imewasili katika mji mkuu wa nchi hiyo Bangui. Vifaa hivyo vimetolewa na Umoja wa Mataifa na wadau wake ukiwemo Muungano wa Ulaya, EU,  na ni kwa ajili ya uchaguzi wa Rais na wabunge uliopangwa kufanyika nchini humo mwezi Desemba mwaka huu.