Kila saa mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi unaongezeka:Guterres

9 Septemba 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi unazidi kuwa mbaya zaidi kila saa.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari hii leo mjini New York katika uzinduzi wa ripoti ya "mshikamano katika sayansi 2020" uliofanyika kwa njia ya mtandao pamoja na shirika la utabiri wa hali ya hewa duniani WMO, Guterres amesema ripoti hiyo iliyohusisha wadau mbalimbali inamulika maendeleo ya kisayansi kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Ameongeza kuwa inaainisha mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi ambao sasa unakuwa mbaya zaidi kila saa, "ndio uchumi umedorora kwa sababu ya janga la corona au COVID-19, lakini ongezeko la joto duniani halijasita. Kama ripoti inavyoonyesha gesi chafuzi ya viwandani imefikia kiwango kipya cha juu kabisa mwaka 2020. Mara ya mwisho kiwango kuwa cha juu kama hiki ilikuwa kati ya miaka milioni 2.6 na milioni 5.3 iliyopita katika zama za Pliocene wakati ambapo kulikuwa na miti kwenye ncha ya Kusini ya dunia na kina cha maji ya bahari kilikuwa juu mita 20."

Mambo yanaenda mrama

Katibu Mkuu amesema miaka mitano tangu kutiwa saini kwa mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi utakuwa ni wakati wenye joto kali katika historia ya binadamu kuwahi kurekodiwa ambapo wastani wa joto ni nyuzi joto 1.1°C  juu ya ilivyokuwa kabla ya mapinduzi ya viwanda.

Ripoti hiyo ya Antonio Guterres na Mkurugenzi Mkuu wa WMO Profesa Talaas inatoa onyo kwamba kuna nafasi kubwa ya kufikia kiwango cha joto cha nyuzi joro 1.5°C  katika miaka mitano ijayo.

Na kwa wakati huohuo kiwango cha barafu baharini Actic na Antarctic (Ncha ya Kaskazini na Kusini) kimekuwa chini ya wastani na kiwango cha kina cha bahari kimezidi kuongezeka kutokana na kuyeyuka kwa barafu.

Ripoti imesema takwimu mpya kwa ajili ya Greenland zinaonesha kwamba kwa wastani barafu inapotea kwa gigatani 278 kwa mwaka.

Na kwamba katika miaka mitano ijayo eneo la arctic linatabiriwa kuendelea kuwa na joto mara mbili ya jumla ya kiwango cha kimataifa.

Malengo yako njiapanda

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya pamoja dunia inakwenda mrama katika kutimiza malengo ya mkataba wa Paris wa kuhakikisha kiwango cha joto kimataifa hakiongezeki zaidi ya nyuzijoto 1.5 Celsius.

Viongozi hao wamesisitiza kwamba, "kama inavyosisitiza ripoti hii kufunga kila kitu kwa muda mfupi sio mbadala wa hatua endelevu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, tunahitaji kutimiza malengo ya makubaliano ya mkataba wa Paris. Athari za kushindwa kwetu kufanya hivyo kushughulikia dharura ya mabadiliko ya tabianchi ziko kila kona. Kiwango kikubwa cha ongezeko la joto, moto mkubwa wa nyikani, mafuriko na ukame. Na changamoto hizi zitazidi kuwa mbaya zaidi".

Ripoti imeonyesha kuwa kutokana na uchafuzi mkubwa wa hewa uliofanyika hapo kabla, dunia imefungwa katika ongezeko zaidi la joto.

"Hakuna muda wa kuchelewesha mambo endapo tunataka kupunguza kasi ya mwenendo huu na kudhibiti ongezeko la joto lisizidi nyuzijoto 1.5 C. Hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ndio njia pekee ya kuhakikisha kwamba dunia yetu ni mahali ambapo kizazi hiki na vizazi vijavyo vinaweza kuishi."

Barafu ikielea juu ya maji katika eneo la Prince Gustav Antarctica
WMO/Gonzalo Javier Bertolotto Quintana
Barafu ikielea juu ya maji katika eneo la Prince Gustav Antarctica

 

Sayansi ndio jawabu mujarabu

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu ripoti imeweka bayana kwamba iwe tunakabiliana na janga la kiafya au mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi  ni wazi kwamba tunahitaji sayansi, mshikamano na maamuzi ya suluhu muafaka.

Ameongeza kuwa, "tuna chaguo , kuendelea na mazoea ambayo yatatutumbukiza kwenye zahma zaidi au tunaweza kutumia fursa ya kujikwamua kutoka kwenye janga la corona au COVID-19 kutoa fursa ya kuiweka dunia katika njia endelevu inayohitajika. Na ndio maana nimetoa wito wa hatua sita muhimu za kuchukuliwa kutuweka katika mwelekeo wa kujikwamua."

Mosi: wakati tunatumia kiwango kikubwa cha fedha kujikwamua na corona ni lazima kuunda ajira mpya na biashara kupitia mabadiliko yanayojali mazingira.

Pili: Mahali ambako fedha za walipa kodi zinatumika kunusuru biashara , zinahitaji kuunganishwa na kufikia ajira endelevu na zinazozingatia ulinzi wa mazingira.

Tatu: Mwelekeo wa uchumi lazima ubadilike kutoka uchafuzi na kuingia kwenye uchumi unaojali mazingira na kuzifanya jamii na watu wake kuwa na mnepo.

Nne: Fedha za umma zitumike kuwekeza katika mustakabali na sio zama za kale, na kuingia katika sekta endelevu na miradi itakayosaidia kulinda mazingira na kudhibiti mabadiliko ya tabianchi.

Tano: Ruzuku katika mafuta kisukuku lazima ikome, wachafuzi wa mazingira lazima walipe gharama ya uchafuzi wao na marufuku kujenga mitambo mipya ya makaa ya mawe. Hatari na fursa lazima vijumuishwe katika mifumo ya fedha , pamoja na masuala ya uwekaji wa sera za umma na miundombinu.

Sita na mwisho: Tunahitaji kufanyakazi pamoja kama jumuiya ya kimataifa. Misingi hii sita ni muongozo muhimu wa kujikwamua vyema amesema bwana. Guterres.

 "Wakati tunajitahidi kupambana na janga la COVID-19 na mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi , ninawataka viongozi wote kutambua ukweli katika ripoti hii na kushikamana kuunga mkono sayansi na kuchukua hatua za haraka dhidi ya mabadiliko ya tabianchi."

 

 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter