UNMISS kujiondoa taratibu vituo vya ulinzi raia ambako usalama umeimarika

9 Septemba 2020

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, David Shearer, amesema hakuna mtu yeyote atakayefurushwa kwenye vituo vya  ulinzi wa raia, POC,  vilivyofungua milango yake wakati ghasia zilipozuka nchini humo mwaka 2013 kunusuru raia waliokuwa wanasaka maeneo salama.
 

Bwana Shearer amesema hayo huko Juba, Sudan Kusini wakati huu ambapo ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNMISS ambaye yeye ndiye mkuu wake, umepanga kuyakabidhi kwa serikali baada ya hali ya utulivu kurejea kwenye maeneo waliyokimbia raia hao miaka 7 iliyopita.

Bwana Sherer amesema kuwa miaka 7 baada ya kuanzishwa kwa vituo hivyo, hali ya usalama imeimarika na wakazi wa vituo hivyo sasa wanatembea kwa uhuru kati ya kambi hiyo na mijini ili kushiriki shughuli za kawaida ikiwemo masomo ya shule, Chuo Kikuu, kufanya manunuzi au kufanya kazi.

“Vituo vya ulinzi wa raia, au POC, vilianzishwa kwa ajili ya kulinda watu waliokuwa hatarini, na vituo hivyo vimetoa huduma hiyo kwa watu makabila mbalimbali, kwa miaka kadhaa, lakini leo hii, wengi wao wanasalia humo ili wapate huduma,”  amesema Mkuu huyo wa UNMISS.

Kituo cha Umoja wa Mataifa cha kulinda Raia, Wau, Sudan Kusini.
UN
Kituo cha Umoja wa Mataifa cha kulinda Raia, Wau, Sudan Kusini.

Kwa sasa UNMISS inasema ghasia za kisiasa zimepungua kufuatia kutiwa saini kwa makubaliano mapya yaliyowezeshwa kuundwa kwa serikali mpya ya Sudan n taratibu UNMISS imeanza kuondoa wanajeshi na polisi wake kutoka vituo vya ulinzi wa raia huko Bor na Wau na itaendelea kufanya hivyo katika vituo vingine.

Amesema kuondolewa walinda amani hao kutoka maeneo ambako ghasia zimepungua, kunatoa fursa ya kuimarisha doria katika maeneo hatari zaidi kama vile Jonglei.

Amesisitiza kuwa pindi walinda amani watakapoondoka vituo hivyo vya ulinzi wa raia, vituo hivyo vitakuwa na majukumu mengina na badala ya kulindwa na Umoja wa Mataifa chini ya sheria za kimataifa, vitakuwa vituo vya kawaida vya wakimbzi wa ndani chini ya mamlaka ya Sudan Kusini.

Hata hivyo ametanabaisha, “hakuna mtu yeyote atakayefurushwa au kutakiwa kuondoka pindi UNMISS itakapoondoka, na huduma za kibinadamu zitaendelea. Ni kwamba vituo hivyo havitakuwa tena chini ya mamlaka yetu bali kama vilivyo vituo vingine vya wakimbizi wa ndani Sudan Kusini, basi vitakuwa chini ya serikali. Itakuwa ni wajibu wa serikali kutafuta maeneo kwa ajili ya wakimbizi hao au iwasaidie warejee nyumbani au wale ambao nyumba zao zinakaliwa na watu wengine.”
 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter