Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 yaweza futa mafanikio ya kupunguza vifo vya watoto wachanga- Ripoti 

Mtoto huyu mchanga hana hofu ya kupatiwa chanjo, huduma ambayo ni muhimu ili kumkinga dhidi ya magonjwa yanayoweza kusababisha vifo. Picha hii ya mwezi Mei mwaka 2020 imechukuliwa kwenye kitu cha afya cha Moussadougou nchini Côte d'Ivoire.
UNICEF/Frank Dejongh
Mtoto huyu mchanga hana hofu ya kupatiwa chanjo, huduma ambayo ni muhimu ili kumkinga dhidi ya magonjwa yanayoweza kusababisha vifo. Picha hii ya mwezi Mei mwaka 2020 imechukuliwa kwenye kitu cha afya cha Moussadougou nchini Côte d'Ivoire.

COVID-19 yaweza futa mafanikio ya kupunguza vifo vya watoto wachanga- Ripoti 

Afya

Ripoti mpya iliyotolewa leo na mashirika ya Umoja wa Mataifa na taasisi zake, imeonesha kuwa mafanikio yaliyopatikana takribani miongo mitatu katika kuepusha vifo vya watoto wachanga yanaweza kufutwa na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa. 

Ikiwa na makadirio mapya ya vifo vya watoto wachanga, ripoti hiyo inasema kuwa idadi ya vifo imepungua kutoka milioni 12.5 mwaka 1990 hadi vifo milioni 5.2 mwaka wa 2019. 

Hata hivyo COVID-19 imevuruga kwa kiasi kikubwa huduma za afya zikiwemo zile za chanjo na huduma za mama na mtoto, imesema ripoti hiyo iliyoandaliwa na shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, lile la kuhudumia watoto, UNICEF, Benki ya Dunia na Idara ya Uchumi na kijamii ya Umoja wa Mataifa. 

Picha ya mtoto mwenye furaha akiwa kwenye kituo cha kulea watoto kilichoko wilaya ya Iganga nchini Uganda.
UNICEF/Proscovia Nakibuuka
Picha ya mtoto mwenye furaha akiwa kwenye kituo cha kulea watoto kilichoko wilaya ya Iganga nchini Uganda.

Mafanikio yaliyopatikana 

Kwa miaka 30 iliyopita, huduma za afya za kinga dhidi ya magonjwa yanayozuia vifo vya watoto kama vile, mtoto kuzaliwa njiti, kuzaliwa na uzito mdogo, matatizo wakati wa kujifungua, vichomi, kuhara, malaria pamoja na huduma za chanjo, vimekuwa na mchango mkubwa katika kuokoa maisha ya mamilioni ya watoto. 

Hivi sasa nchi ulimwenguni kote zinakumbwa na mvurugiko mkubwa wa huduma za mtoto na uzazi, kama vile huduma za kliniki kabla na baada ya kujifungua, chanjo na hii inatokana na rasilimali nyingi kuelekezwa katika vita dhidi ya COVID-19 pamoja na wajawazito kuhofia kupata maambukizi iwapo watakwenda kusaka huduma za kliniki na chanjo. 

Akizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore amesema kuwa, “jamii ya kimataifa imetoka mbali sana kutokomeza vifo vya watoto vinavyoweza kuepukika kiasi kwamba iruhusu COVID-19 ituondoe kwenye mwelekeo wetu. Pindi watoto wanakosa huduma za afya kwa sababu mfumo wa afya umezidiwa uwezo, na pindi wanawake wanapohofia kujifungulia hospitali kwa sababu ya hofu ya maambukizi, nao pia wanaweza kuwa waathirika wa COVID-19. Bila uwekezaji wa haraka kuanzisha upya huduma za afya zilizovurugika, mamilioni ya watoto, hususan wale wachanga wanaweza kufariki dunia.” 

Naye Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema kuwa suala kwamba leo hii watoto wengi zaidi wanaozaliwa wanaweza kusherehekea mwaka mmoja wa kuzaliwa kuliko wakati wowote ule katika historia, ni ala tosha ya mafanikio yaliyopatikana kwa kuweka mbele afya na ustawi wa binadamu. 

Leo hii katu tusikubali COVID-19 ifute mafanikio ya watoto wetu na vizazi vijavyo. Badala yake ni wakati wa kutumia kile tunachofahamu ili kuokoa maisha na kuimarisha uwekezaji wetu, mnepo na mifumo yetu ya afya,” amesema Dkt. Tedros. 

Tafiti zilifanyika vipi? 

UNICEF ilifanya utafiti wakati wa msimu huu wa kiangazi katika mataifa 77 na kubaini kuwa takribani asilimia 68 ya mataifa hayom, huduma zao za afya zilivurugwa  hususan zile za chanjo. Halikadhalika asilimia 63 ya nchi hizo iliripoti kuvurugika kwa huduma za kwa wajawazito ilhali asilimia 59 walikumbwa na changamoto kwenye huduma za baada ya mtoto kuzaliwa. 

Kwa upande wake WHO iliendesha utafiti katika mataifa 105 na kubaini kuwa katika asilimia 52 ya nchi husika, huduma za afya kwa watoto wagonjwa zilivurugika huku asilimia 51 ziliripoti matatizo kwenye ufuatiliaji na usimamizi wa huduma dhidi ya utapiamlo. 

Kwa mujibu wa tafiti hizo, nchi zilizoshiriki zilitaja sababu kuu ya kuvurugika kwa huduma za afya kuwa ni pamoja na hofu ya maambukizi ya COVID-19, vizuizi vya safari, kusitishwa au kufungwa kwa vituo vya afya, idadi ndogo ya wahudumu wa afya baada ya wengi wao kuelekezwa kwenye COVID-19 au uhaba wa vifaa vya kujikinga kama vile barakoa na glovu. 

Miongoni mwa nchi zilizoathirika zaidi ni  Afghanistan, Bolivia, Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, Libya, Madagascar, Pakistan, Sudan na Yemen.