Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yafafanua suala la ulinzi wa Dkt. Mukwege

Dkt. Denis Mukwege, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel 2018 na muasisi na mwendeshaji wa kliniki ya Panzi, Bukavu jimboni Kivu  Kusini nchini DRC.
ONU Info
Dkt. Denis Mukwege, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel 2018 na muasisi na mwendeshaji wa kliniki ya Panzi, Bukavu jimboni Kivu Kusini nchini DRC.

UN yafafanua suala la ulinzi wa Dkt. Mukwege

Amani na Usalama

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO, umesema bado umejizatiti katika kuhakikisha usalama wa Dkt. Denis Mukwege pamoja na kliniki yake ya Panzi iliyoko Bukavu, jimbo la Kivu Kusini, mashariki mwa taifa hilo.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema hayo leo akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani kwa njia ya video, kwa kuzingatia ripoti za za hivi karibuni zilizodai kuwa MONUSCO imesitisha ulinzi wa Dkt. Mukwege ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel kwa mwaka 2018.

Bwana Dujarric akinukuu taarifa ya MONUSCO amesema, “ijapokuwa idadi ya wagonjwa virusi vya Corona, au COVID-19 miongoni mwa walinda amani wetu imekuwa na athari kwenye operesheni zetu, bado tunaendelea kufanya kazi kwa karibu na Dkt. Mukwege, mamlaka za DR na wadau wa kimataifa kuhakikisha kuwa mahitaji yake ya usalama na yale ya kliniki yake yanashughulikiwa kwa ufanisi na kwa uendelevu.”

Amesema kwa MONUSCO kuweza kuzingatia hilo, ni lazima waendelee kuimarisha uwezo wa polisi wa kitaifa kwa msaada wa ujumbe huo na wadau wengine wa kimataifa.

Hata hivyo Bwana Dujarric amekumbusha kuwa usalama wa wananchi wa DRC ni jukumu la mamlaka za kitaifa, lakini MONUSCO inatoa msaada kwa kadri ya uwezo wake.

Mapema hii leo msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, Rupert Colville akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi amesema ripoti za vyombo vya habari kuwa walinda amani wameacha kumlinda Dkt. Mukwege hazina ukweli wowote huku akisisitiza kuwa kwa sasa kutokana na changamoto za kirasilimali, hakuna kikundi cha kudumu cha ulinzi lakini walinda amani wanaendelea kupatiwa mafunzo na doria zinaendelea.

Hivi karibuni kumekuwepo na ripoti za vitisho vya mauaji dhidi ya Dkt. Mukwege ambaye amekuwa mstari wa mbele siyo tu kutibu manusura wa ukatili wa vitendo vya ubakaji, bali pia akitaka watekelezaji wa vitendo hivyo wafikishwe mbele ya sheria.