Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wazazi na wanafunzi washika hatamu kwenye masomo Uganda wakati huu wa Corona

Daniel Mungoci mwenye umri wa miaka 16 akiwa anajisomea nyumbani wakati huu ambapo bado shule zimefungwa nchini Uganda kutokana na COVID-19.
UNICEF/Francis Emorut
Daniel Mungoci mwenye umri wa miaka 16 akiwa anajisomea nyumbani wakati huu ambapo bado shule zimefungwa nchini Uganda kutokana na COVID-19.

Wazazi na wanafunzi washika hatamu kwenye masomo Uganda wakati huu wa Corona

Utamaduni na Elimu

Gonjwa wa Corona au COVID-19 likiendelea kusababisha baadhi ya nchi kufunga shule na vyuo na hivyo wanafunzi kulazimika kusomea majumbani, walimu, wazazi na wanafunzi nchini Uganda, wamezungumzia changamoto wanazokumbana  nazo.

Kwa Mwalimu Irene wa shule ya msingi ya Clarke iliyoko jijini Kampala nchini Uganda yeye anasema kuwa, “serikali ilipoamua kufunga shule, hilo lilikuwa jambo la kushangaza na ilkuwa ni mazingira tofauti kabisa kwa wazazi na wanafunzi. watoto wetu hawakuwa wamezoea kuchapa maneno. Wazazi wengi hawakuwa na kompyuta mpakato. Badala yake walikuwa na simu za rununu, na ndipo tukaone tutumie apu ya WhatsApp” 

Hata hivyo bado kuna changamoto,  Edrien mwanafunzi katika shule ya Clarke mwenye umri wa miaka 11 anasema kuwa changamoto kubwa ni kwamba hana simu ya rununu. 

Kwa kuwa familia yao haina simu ya rununu, baba mzazi wa Edrien ambaye ni dereva wa bodaboda na sasa hafanyi kazi kutokana na COVID-19, analazimika kwenda shuleni kuchukua kazi za shule za mwanae. 

Mwalimu Irene anasema kuwa, “Robert ni miongoni mwa wazazi, na anaishi mbali na shule kwa hiyo ni lazima asafiri umbali mrefu. Kwa hiyo anasaidia wanae nyumbani kwa kuwa wanashindana na wanafunzi wengine” 

Kwa Edrien awali alikuwa na hofu kuwa kitendo cha baba yake kwenda kufuata nyaraka shuleni, angaliwaletea virusi vya Corona, lakini haikuwa hivyo na zaidi ya yote anasema kuwa anafurahi kwa kuwa baba yake anamsaidia sana.

Sasa masomo yanaendelea na baba anamuuliza Edrien atafute neno jipya kwenye kamusi na analiona na kisha Robert ambaye ni baba mzazi anasema ”unafahamu katika huu ulimwengu, kama hujaelimika, maisha ni magumu mno.  Kwa hiyo lazima ujitahidi sana ili watoto wako waende shule kwa maisha mazuri ya baadaye. Shule ni mbali, natumia kati ya dakika 45 hadi 50 kufika shule. Lakini shule ile ina elimu bora.”