Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlipuko wa nzige Kusini mwa Afrika watishia uhakika wa chakula:FAO 

Nzige wa Jangwani ambao kwa muda wamevamia maeneo ya Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika, sasa wamevamia nchi za kusini mwa Afrika.
© FAO/Haji Dirir
Nzige wa Jangwani ambao kwa muda wamevamia maeneo ya Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika, sasa wamevamia nchi za kusini mwa Afrika.

Mlipuko wa nzige Kusini mwa Afrika watishia uhakika wa chakula:FAO 

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO leo limeonya kwamba mlipuko wa nzige uliozuka Kusini mwa afrika unatishia uhakika wa chakula na limetaka hatua zichukulie haraka kuzuia janga kubwa la kibinadamu na kunusuru mamilioni ya watu Botswana, Namibia, Zambia na Zimbabwe. 

FAO hivi sasa imezindua mkakati wa hatua za kudhibiti wimbi hilo la nzige ambapo watu takriban milioni 7 katika nchi hizo nne ambao bado wanajikwamua kutokana kwenye ukame wa mwaka 2019 na sasa athari za kiuchumi na kijamii za janga la corona au COVID-19 huenda wakakabiliwa hali mbaya zaidi ya kutokuwa na uhakika wa chakula na lishe. 

FAO inashirikiana na jumuiya ya maedeleo kwa nchi za Kusini mwa afrika SADC na shirika la kimataifa la kudhibiti nzige wekundu kwa nchi za katikati na Kusini mwa Afrika (IRLCO-CSA) kusaidia serikali za nchi zilizoathirika kudhibiti nzige hao. 

Patrice Talla mratibu wa kikanda wa FAO Kusini mwa Afrika amesema, “hata kwa hatua ambazo tayari zimeshachukuliwa kuwadhibiti nzige hao bado ni tishio . Baadhi ya maeneo yaliathirika zaidi ni vigumu kuyafikia, tunahitaji kuzisaidia serikali hizi nne. SADC na mashirika wadau kama IRLCO-CSA kuwadhibiti wadudu hawa na kulinda maisha ya watu masikini.” 

Tishio kwa uhakika wa chakula 

Mlipuko huu wa nzige Kusini mwa Afrika FAO inasema ni tofauti na lule wa nzinge wa jangwani unaoendelea Afrika Mashariki. 

Nzige ni miongoni mwa wadudu waharibifu zaidi duniani kundi moja linaweza kuwa na mamilioni ya nzige wakubwa na sasa kuna makundi mengi Kusini mwa Afrika. Na kundi moja la nzige chakula linachokula kwa siku moja ni sawa na milo ya watu 2,500, linamaliza mazao na malisho ya mifugo kwa muda wa saa chache.  

Nchini Botswana baadhi ya wakulima wadogo wadogo wamepoteza mazao yao yote wakati wa mwanzo wa mlipuko wa nzige hawa wa kuhamahama wa afrika, na wakati msimu ujao wa upanzi ukijongea wadudu hao wanatishia mustakabali wa jimbo linalolisha taifa hilo la Pandamatenga ambako asilimia kubwa ya mtama ambao ni chakula kikuu cha nchi hiyo unalimwa, na litakuwa janga kubwa endapo hatua hazitochukuliwa haraka .

Nchini Namibia mlipuko wa awali ulianzia kwenye uwanda wa Zambezi na sasa makundi hayo ya nzinge yamesambaa katika kanda muhimu za kilimo. Sawa na Zambia FAO inasema nzige wamesambaa haraka na wanaathiri mazao na malisho ya mifugo. 

Nchini Zimbabwe makundi hayo ya nzige yalivamia maeneo mawili kwanza katika wilaya ya Chiredzi na sasa yamehamia katika jimbo la Manicaland.  

Athari za nzige hao kwa mazao zitazzidisha hali ya kutokuwa na uhakika wa chakula katika jamii ambazo tayari zimeathirika na mafuriko, ukame na athari za janga la COVID-19. 

Juhudi za pamoja zahitajika 

FAO leo imezindua mradi wa dharura wa Kusini mwa afrika kukabiliana na nzige hao na maandalizi ambao unafadhiliwa na program ya ushirikiano wa kiufundi ya FAO. 

Mradi huo utakaogharimu dola nusu milioni utajikita na hatua za dharura katika maeneo yaliyoathirika zaidi na kuimarisha uratibu na kupeana taarifa miongoni mwa nchi zilizoathirika. 

Pia utawezesha ufuatiliaji wa mwenendo wa nzige hao kwa njia ya anga na shughuli za ramani ya kuliko athirika na kutoa msaada wa kiufundikwa ajili ya kuanzishwa mfumo wa kitaifa wa ufuatiliaji na vitengo vya udhibiti wa nzige.