Ghasia mpya Kasai zinaweza kuchochea wimbi jipya la ukimbizi- UNHCR 

4 Septemba 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, leo limeonya kuwa ghasia mpya zinazoibuka katika eneo la Kasai nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, zinaweza kuibua wimbi kubwa la ukimbizi iwapo hali ya sasa haitaimarishwa. 

Msemaji wa UNHCR Babar Baloch, akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo amesema kuwa eneo hilo limekuwa na utulivu kidogo lakini katika mwezi uliopita zaidi ya watu 24,000 walikimbia makwao kutokana na mizozo mitatu tofauti ikihusiana na ardhi, kugombea rasilimali, ukabila na mapigano baina ya vikundi tofauti vilivyojihami na jeshi la serikali. 

Amesema idadi kubwa ya waliokimbia makwao wamesaka  hifadhi katika maeneo ya mpakani mwa jimbo la Demba huko Kasai Kati na Mweka eneo la Kasai, akikumbusha kuwa ghasia za mwaka 2017 zilisababisha ukimbizi wa ndani kwa watu milioni 1.4 nchini DRC ambapo wengine 35,000 walikimbilia Angola na kwamba, “wakimbizi wa sasa wameripoti kuwa katika wiki za karibuni kumekuwepo na mauaji, ubakaji, mateso, uporaji wa mali na nyumba kuchomwa moto. Makumi ya watu wamewasili wakiwa na majeraha. Kuna watoto, wanawake na wazee wengi miongoni mwa wakimbizi wa ndani.Huko Katende, eneo la Kasai Kati, mapigano baina ya jamii mbili kwenye madini na mbao yalipamba moto mwezi wote wa Agosti na takribani watu 1,000 wamejikuta wakimbizi.” 

Amesema kwa sasa UNHCR inasajili wakimbizi hao na wale wanaowapatia hifadhi, jamii ambazo hata zenyewe ni maskini na zinakabiliwa na kiwango cha juu cha utapiamlo. 

Halikadhalika wanawapatia msaada manusura wa ukatili wa kingono na wamesambaza vifaa muhimu kama vile blanketi, sabuni, vifaa vya jikoni kwa watu zaidi ya 4,000 huku wengine wakipatiwa fedha ili kukidhi mahitaij ya msingi. 

Hata hivyo amesema UNHCR inaendelea kufuatilia hali ilivyo ili kushughulikia mahitaij ya manusura wa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, huku ikitaka hatua mpya za kurejesha amani Kasai na kumaliza mvutano. 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud