Tudumishe hatua za pamoja dhidi ya COVID-19:Rais wa Baraza Kuu la UN 

3 Septemba 2020

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo amezichagiza nchi wanachama kuhimiza hatua za pamoja katika kupambana na janga la corona au COVID-19 katika kikao cha kwanza cha ana kwa ana tangu mwezi Machi mwaka huu. 

Tijani Muhammad-Bande akizungumza moja kwa moja kwenye ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York hii leo ikiwa ni karibu miezi sita ya kufanya vikao kwa njia ya mtandao kuzuia kusambaa kwa maambukizi ya COVID-19 amewataka wachama waliohudhuria kuhakikisha wanashirikiana ili kupambana na janga hili linaloendelea kuitikisa dunia. 

“Ingawa hatujakutana kwenye ukumbi huu tangu mwezi Machi , wajumbe walioko hapa New York wamekuwa wakifanyakazi bila kuchoka kutekeleza maadili na misingi iliyowekwa na katiba ya Umoja wa Mataifa huku wakipambana na janga la COVID-19.” 

Kuhakikisha kazi inaendelea 

Bwana. Muhammad-Bande ambaye ameliita Baraza Kuu kama chombo cha maamuzi cha Umoja wa Mataifa amesema kwamba kimeendelea na kazi za shirika huku kikifanya kila njia kudumisha ushirikiano kwa lengo dunia kujijenga vyema baada ya janga hili. 

Bwana.Muhammad-Bande amekipongeza chombo hicho muhimu kwa kuona mbali katika kupitisha na kuongeza uamuzi namba 74/544 ambao uliruhusu wanachama kupitisha maamuzi  na maazimio zaidi ya 70 na pia kuchagua wenyevit wa kamati mbalimbali kwa ajili ya kikao cha kihistoria cha 75 cha Baraza Kuu.  

“Hili limehakikisha kazi inaendelea katika masuala mbalimbali ya muhimu”. 

Amelikumbusha Baraza kuhusu umuhimu wa kuzingatia masualaya kujitenga kuepuka maambukizi kwenye chaguzi zinazokuja za Rais wa Baraza la kiuchumi na kijamii la Umoja wa Mataifa ECOSOC na Baraza Kuu lenyewe lakini pia wajumbe wapya wa Baraza la Usalama. 

“Tulitumia njia ya mtandao kuwaleta pamoja wadau wote kutoka kote duniani katika siku ya katiba ya Umoja wa Mataifa, na kwa mara nyingine katika kusikiliza maadhimisho ya 25 ya mkutano wan ne wa dunia wa wanawake, asante sekretariati kwa kujizatiti kwenu.” 

Miaka 75 na kuendelea 

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amepongeza kazi ya majadiliano ya kimataifa kuhusu azimio la maadhimisho ya 75 ya Umoja wa Mataifa. Pia amezishukuru nchi wanachama ambazo zimeonyesha uongozi imara katika kukabiliana na janga la kimataifa la COVID-19 kwa kupitisha maazimio mawili yaliyoungwa mkono kwa kiasi kikubwa  yanayotoa wito wa mshikamano na fursa ya kimataifa ya dawa na vifaa tiba. 

Zaidi yah apo amempongeza mwenyekiti wa kamati ya tano inayohusika na masuala ya uongozi na bajeti kwa kutumia njia bunifu ambazo zimeruhusu kikao kinachoendelea kukamilisha miswada ya mapendekezi 21 na kupitisha bajeti ya dola bilioni 6.5 za operesheni za ulinzi wa amani kwa mwaka wa fedha 2020-2-21. 

“Kazi yenu imehakikisha kwamba Umoja wa Mataifa unaweza kuendelea kufanyakazi mashinani na kukidhi mahitaji ya watu tunaowahudumia.” Amesema kwa fahari kubwa Rais huyo wa Baraza Kuu. 

WHO imeshika usukani 

Rais wa Baraza Kuu amelipongeza pia shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO kwa kuongoza hatua za kupambana na COVID-19 tangu mwanzo wa mlipuko. 

“Mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa umeshikamana kushughlikia mahitaji ya watu tunaowahudumia. Nawapongeza wahudumu wa kibinadamu walioko mashinani na walinda amani wetu ambao wanaendelea kulinda jamii katika mazingira magumu kote duniani.” 

Bwana. Muhammad-Bande amesisitiza umuhimu wa juhudi hizo tunapoanza muongo wa hatua na ifikishaji katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu SDGs, au uwezekano wa kuwa ni muongo wa kujikwamua kutoka kwa janga la COVID-19. 

“Natoa wito kwenu kuhimiza hatua za pamoja za kimataifa sasa ili kutimiza ahadi zetu za ufadili kwa ajili ya maendeleo Tunasalia pamoja katika hili , kama mataifa yaliyoungana. Hebu tuendelee kushikamana na kutimiza malengo haya kwa wote.” 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter