Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunafuatilia vikwazo vya Marekani dhidi ya watendaji wa ICC - UN

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, Fatou Bensouda
ICC
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, Fatou Bensouda

Tunafuatilia vikwazo vya Marekani dhidi ya watendaji wa ICC - UN

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amepokea kwa wasiwasi tamko la hii leo la Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo la kutangaza vizuizi zaidi dhidi ya mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC, Fatou Bensouda na Afisa wa mahakama hiyo.

Tangazo hilo la Pompeo dhidi ya Bensouda na  Phakiso Mochochoko ambaye ni Mkuu wa kitengo cha ICC kinachohusika na masuala ya mamlaka ya kimaeneo ya mahakama hiyo na ushirikiano, linadai kuwa msingi wake ni kwamba ICC katika utendaji wake inazidi kulenga raia wa Marekani.

Wawili hao sasa wanaguswa na vikwazo kwa mujibu wa amri ya rais wa Marekani ya kuzuia mali ya baadhi ya watu wanaohusiana na ICC ya tarehe 11 mwezi Juni mwaka huu wa 2020. Vikwazo hivyo ni pamoja na kuzuia mali zao zilizopo Marekani au zinazohusiana na sheria ya Marekani.

“Tunaendelea kufuatilia kwa karibu kile kinachoendelea kuhusu suala hili. Ushirikiano katiya Umoja wa Mataifa na ICC ni kwa msingi wa makubaliano yaliyoridhiwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 13 mwezi Septemba mwaka 2004. Tutakuwa tunachunguza uwezekano wa wowote wa athari za hatua hii katika kutekeleza makubaliano hayo,” amenukuliwa msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric wakati akizungumza na waandishi wa habari hii leo jijini New York, Marekani.

Msemaji huyo ameongeza kuwa, “kwa mujibu wa taarifa za awali za Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Marekani, tunaamini kuwa vizuizi vyovyote dhidi ya maafisa hao wa ICC vitatekelezwa kwa kuzingatia wajibu wa nchi mwenyeji kwenye mkataba wa makao makuu ya Umoja wa Mataifa.”

Umoja wa Mataifa bado unafuatilia iwapo Bi. Bensouda bado anaweza kusafiri kwenda Marekani kwa mujibu wa mkataba huo wa UN na nchi mwenyeji wa makao makuu ya chombo hicho na kwamba ICC itachunguza ni kwa vipi uamuzi wa leo utaathiri kazi ya mahakama.
Hii si mara ya kwanza kwa Marekani kutangaza vizuizi dhidi ya Bensouda kwani mwezi Machi mwaka 2019, Waziri Pompeo alitangaza kuwa serikali yao haitawapatia vibali vya kuingia nchini Marekani wafanyakazi wa ICC akiwemo Bi. Bensouda, na itafuta vibali ambavyo tayari vimetolewa kwa wafanyakazi wa mahakama hiyo yenye makao yake makuu huko The Hague, Uholanzi.
Ofisi ya Bi. Bensouda ilithibitisha wakati huo kuwa serikali ya Marekani ilifuta kibali cha kuingia nchini humo kwa madai ya kuchunguza harakati za jeshi la Marekani nchini Afghanistan.