Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Familia zinazokimbia mashambulizi Msumbiji zajikuta katika maeneo yaliyoghubikwa na COVID-19 

Wakimbizi wa ndani katika maeneo ya Alto Gingone, Pemba mkoa wa Cabo Delgado, Msumbiji
UN Mozambique/Helvisney Cardoso
Wakimbizi wa ndani katika maeneo ya Alto Gingone, Pemba mkoa wa Cabo Delgado, Msumbiji

Familia zinazokimbia mashambulizi Msumbiji zajikuta katika maeneo yaliyoghubikwa na COVID-19 

Ukuaji wa Kiuchumi

Mashambulizi katika miji na vijiji vya mkoa wa kaskazini mwa Msumbiji wa Cabo Delgado yamezidi na  kuwalazimisha maelfu ya watu kukimbia kwa miguu, boti au barabara kwenda katika makao makuu ya mkoa ambako ni kitovu cha COVID-19 na ambako shirikisho la kimataifa la chama cha msalaba mwekundu ICRC limesaidia kujenga kituo kikubwa cha matibabu kinachofunguliwa rasmi leo, imeeleza taarifa iliyotolewa hii leo na ICRC mjini Maputo. 

Taarifa hiyo ya ICRC inasema familia zimewasili katika mji wa Pemba zikiwa zimechoka na wakiwa na kiwewe baada ya kuondoka katika nyumba zao wakiwa na vitu vichache au bila chochote huku ikitegemewa kuwa kuna uwezekano wa wengine zaidi walioyakimbia mashambulizi katika maeneo ya Mocimboa da Praia na maeneo mengine, kuwasili  katika wiki zijazo.  

Mkuu wa operesheni za ICRC katika mji wa bandari wa Pemba nchini Msumbuji, Raoul Bittel amenukuliwa akisema, “watu wanaoukimbia mzozo wa silaha nchini Msumbiji wamekimbia tishio hili dhidi ya maisha yao na kukumbana na hatari ya COVID-19. Kituo kipya cha matibabu kitasaidia jamii kukabiliana na janga la kiafya lakini familia haziwezi kurejea hadi pale ambapo mapigano yataenda mbali na makazi ya raia.”  

Aidha taarifa hiyo ya shirikisho la kimataifa la chama cha msalaba mwekundu, ICRC imeeleza kuwa hatari ya kuambukizwa ugonjwa wa COVID-19 mjini Pemba, ambako ni moja ya maeneo yenye maambukizi makubwa nchini Msumbiji ni kubwa. Wengi wa watu waliotawanywa wanapata makazi katika familia au ndugu na hivyo kuongeza mzigo juu ya wenyeji wao hao na pia kuongeza hali ya msongamano ambayo inasaidia kusambaa kwa COVID-19 kwa kuwa umbali kati ya mt una mtu unakuwa hauwezekani.  

Dkt Basilio dos Mwelus ambaye ni Mkuu wa Idara ya mipango ya afya katika eneo hilo amesema Decimo Congresso ni kituo kikubwa cha matibabu ya COVID-19 nchini humo na wanategemea hawatakitumia chote kwa sasa lakini wakilazimika kufanya hivyo, wako tayari.  

Vurugu za mara kwa mara zimekuwa zikisumbua jamii katika eneo lenye utajiri wa rasilimali la  Cabo Delgado tangu 2017, lakini zimeongezeka kwa kasi na nguvu katika mwaka huu wa 2020. Miji ambayo hapo awali haikuwa imeguswa na vurugu hizi na hivyo  kutumiwa kama mahali pa kukimbilia kwa wale waliokimbia mashambulio katika maeneo mengi ya vijijini, nayo sasa imeshambuliwa.