Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwalimu mkimbizi ahofia kuwa fursa aliyopata ya kusoma ni finyu kwa wanae na watoto wengine wakimbizi

Wanafunzi wakijifunza katika shule ya msingi na sekondari ya Makod katika kambi ya wakimbizi ya Tierkidi katika eneo la Gambella, Ethiopia.
UNICEF/ Ethiopia/2018/Mersha
Wanafunzi wakijifunza katika shule ya msingi na sekondari ya Makod katika kambi ya wakimbizi ya Tierkidi katika eneo la Gambella, Ethiopia.

Mwalimu mkimbizi ahofia kuwa fursa aliyopata ya kusoma ni finyu kwa wanae na watoto wengine wakimbizi

Wahamiaji na Wakimbizi

Mkimbizi huyo James Tut, ambaye ameshajikuta mkimbizi mara mbili katika maisha yake, alianza masomo ya shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Addis Ababa nchini Ethiopia mwaka 2010 na kuhitimu  mwaka 2014. 

Hakuweza kurudi nyumbani kwa kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilianza Desemba mwaka 2013, na hivyo kusalia kambini Gambella na kuanza kufundisha. 

Hivi sasa ni Mwalimu Mkuu Msaidizi katika moja ya shule nne kwenye kambi ya wakimbizi ya Jewi mjini Gambella nchini Ethiopia. 

Mwalimu huyu anasema kuwa, “kazi yangu inafurahisha sana kwa sababu ni wakati wangu kurudisha huduma kwa jamii. Watoto hawa, ni mustakabali wa nchi yetu, iwapo tutarejea, basi wataendeleza nchi yetu. Lakini iwapo tutasalia wakimbizi hapa, basi ni tatizo kubwa na nina hofu kubwa.” 

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, linasema kuwa kwa mwalimu Tut, ilikuwa ni bahati kwa kuwa alishinda vikwazo vyote na kuhitimu masomo yake ya Chuo kikuu kwa kuwa ni vigumu sana kwa wakimbizi kupata elimu ya juu na takwimu zinaonesha kuwa ni asilimia 3 tu ya wakimbizi duniani ndio wanaopata fursa hiyo. 

Bwana Tut alitumaini kuwa baada ya kumaliza masomo yake ya shahada ya maendeleo ya jamii na uongozi, angaliweza kuajiriwa na serikali ya Sudan Kusini. 

Lakini kuibuka kwa vita kulikuwa ni kikwazo na akajikuta mkimbizi Ethiopia kwa mara ya pili. 

Takwimu zinaonesha kuwa, takribani miaka 7 ya ghasia nchini Sudan Kusini imekuwa janga kwa watoto na vijana. 

Theluthi mbili ya wakimbizi wote wa Sudan Kusini wana  umri wa chini ya miaka 18 na ni asilimia 69 tu wako shule ya msingi ikilinganishwa na asilimia 91 kimataifa. 

Hali inakuwa mbaya zaidi wakipanga ngazi za juu ambapo ni asilimia 13 tu ya watoto wakimbizi wa Sudan Kusini ndio wanaojiunga na elimu ya sekondari ikilinganishwa na asilimia 84 duniani kote. 

Hata hivyo kwa sasa Mwalimu Tut ni ushahidi hai ya kwamba mkimbizi anaweza kufanikisha chochote kile iwapo atapatiwa fursa.